Askofu Dkt. Shoo afungua Warsha ya LCA na OCA Uhuru

Baba Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo Mkuu wa KKKT na Dyosisi ya Kaskazini amefungua  Warsha ya Matokeo ya Tathmini ya Leardership Capacity Assessment (LCA) na Organization Capacity Assessment (OCA) ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini kuelekea Kuunda Mpango Mkakati wa Dayosisi (2023-28) tarehe 21 Machi, 2023 Lutheran Uhuru Hotel & Conference Centre.

Akifungua kwa neno Warsha hiyo iliyohudhuriwa na viongozi wa Dayosisi, Wadiri na Wakuu wa  Majimbo, Askofu Dkt. Shoo alisoma neno kutoka Mhubiri 9:10, “Lo lote mkono wako utakalolipata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako; kwa kuwa hakuna kazi, wala shauri, wala maarifa, wala hekima, huko kuzimu uendako wewe.”

Katika ujumbe wake alikazia kwamba, ni wajibu wa kila mtumishi wa Dayosisi na Msharika kuhakikisha kwamba, katika kila jambo analofanya  katika maisha yake ya kiroho, kiuchumi, kijamii, kielimu n.k. basi afanye kila kitu kwa moyo, nguvu, bidii na iwe kwa wakati mwafaka. Hii ni kwa sababu, muda tulionao una mwisho, kwa hiyo ni muhimu kutenda kila jambo kwa uaminifu.

Alisema hatutakiwi kufanya jambo lolote kwa ulegevu bali tunapaswa kufanya kwa bidii, maarifa na kwa moyo.

“Hakuna aliyefanya kazi yake kwa bidii akaacha kuona matunda mazuri; Tunatumiaje muda wetu na vipawa vyetu? Tunapaswa kutambua muda tulionao una mwisho na muda ukishapita haurudi tena. Lile ambalo unapaswa kulifanya leo lifanye maana ukishindwa kulifanya utambue haututapata fursa ya kurudisha muda na kulifanya kwa wakati ule”.Alisema

Baada ya neno na sala, Katibu Mkuu Mhandisi Zebadiah S. Moshi, alitoa maelezo ya awali kuhusu zoezi la LCA & OCA). Kisha kabla ya kuwakaribisha wataalamu wa Mpango Mkakati, aliwakaribisha washiriki wote wa warsha kuimba pamoja wimbo TMW. 324 unaosisitiza umuhimu wa kufanya kazi kwa bidii kungali mapema kwani usiku waja upesi.

Baada ya wimbo huo, aliwakaribisha wataalamu wa Mpango Mkakati Dkt. Godwin Kimaro na Dkt. Moses Matei kuwasilisha matokeo ya zoezi la LCA na OCA. Zoezi hilo lilifanyika kama hatua za awali za kuelekea kuunda Mpango Mkakati wa Dayosisi wa miaka mitano (5) kuanzia 2023-2028.

Zoezi hili la LCA na OCA lilijumuisha washarika wote wa Dayosisi kupitia uwakilishi Kimajimbo kadhalika taasisi zote za Dayosisi zinazojumuisha taasisi za Afya, Elimu na vituo vya kiuchumi. Kwa njia hii, kumefanya uundaji wa Mpango Mkakati wa Dayosisi 2023-2028 kuwa shirikishi zaidi.

Akitoa maelezo ya awali kuhusu zoezi zima la LCA, OCA na faida zake, mtaalamu wa Mpango Mkakati Dkt. Godwin Kimaro alitaja mambo 8 muhimu kati ya mengine ya LCA na OCA kuwa ni; zinaisaidia taasisi na watumishi kujifahamu kwani usipojifahamu huwezi kujisahihisha, Pili kiila siku kuna kitu cha kujifunza katika maisha binafsi kadhalika maisha ya taasisi na tatu ni muhimu kila kinachofanywa na mtu binafsi na taasisi kiwe na vigezo vya kupimika kwani kitu ambacho hakiwezi kupimwa ni sawa na kusema hakijafanyika.

Jambo la nne alitaja kuwa ni  muhimu wakati wote kuepuka kutengeneza migogoro kwa sababu tu, tunachagua kutumia suluhusho rahisi. Mathalani, badala ya kuimarisha mfumo wa mawasiliano kati ya A na C, tunatengeneza nafasi ya B, tano alisema ni muhimu kila kitu kifanyike kwa usahihi pasipokuleta migongano ya madaraka/ mamlaka au majukumu sita ni muhimu kuhusisha na kujumuisha wataalamu katika kutatua changamoto kwa uendelevu wa mtu binafsi na taasisi pia na saba Baada ya LCA & OCA mtu binafsi kadhalika taasisi inaweza kuanza kuchukua hatua ya kurekebisha panapotakiwa kurekebishwa na kuendeleza yale yanayotakiwa kuendelezwa hata kabla ya kuundwa waraka wa Mpango Mkakati.

Jambo la nane Dkt. Kimaro alisema kutokana na LCA & OCA hatua inayofuata ni kuunda Mpango Mkakati wa Dayosisi unaoendana na Mpango Mkakati wa KKKT lakini unaozingatia pia mahitaji ya kipekee ya Dayosisi kama maeneo ya matokeo kutokana na LCA & OCA.

Ask. Dkt. Fredrick O. Shoo Mkuu wa KKKT, DK (wa tatu kutoka kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Warsha ya Matokeo ya Tathmini ya LCA na OCA. Pamoja naye (wa pili kutoka kulia) ni Msd. Ask Mch. Deogratius Msanya, (wa kwanza kutoka kushoto) ni Katibu Mkuu Mhandisi Z.S. Moshi na waliosimama kulia na kushoto kwa Mkuu wa KKKT, DK ni wataalamu wa Mpango Mkakati, Dkt. Godwini Kimaro (kulia) na Dkt. Onesmo Matei (kushoto).