Ni siku ya michezo kwa watoto wenye ulemavu wa akili wanaohudumiwa na Building a Caring Community (BCC), ilifanyika Agosti 27, 2021 katika viwanja vya Uhuru Lutheran Hotel& Conference Centre Shanti Town Moshi, ambapo watoto zaidi ya 100 walishiriki michezo ya aina mbalimbali iliyoandaliwa na kituo hicho kilicho chini ya Idara ya Udiakonia ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini.
Siku hiyo maalumu kwa ajili ya michezo kwa watoto hao hufanyika mara moja kila mwaka ambayo hufadhiliwa na wahisani toka shirika la Mosaic International la Marekani linalojishughulisha na kuwahudumia watoto wenye mtindio wa ubongo wakishirikiana na KKKT Dayosisi ya Kaskazini.
Mashindano hayo yanajulikana kama Field Day yanahusisha michezo ya aina mbalimbali ikiwemo mpira wa miguu, muziki na michezo mingine yalifunguliwa na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya BCC Mch. James Nkya.
Akifungua michezo hiyo Mch.Nkya alisema tangu kuanzishwa kwa BCC kutoa huduma katika sharika za Manispaa ya Moshi mwaka 2007, kumekuwa msaada mkubwa kwani watoto wengi wamefunguka na hali zao kuwa bora ukilinganisha na walivyokuwa wakiachwa nyumbani bila uangalizi wa kitaalam.
“Tangu 2007 BCC ilipoanzishwa tumeona mkono wa Mungu kwa jinsi alivyowafungua watoto hawa kwa kiasi kikubwa. Tunaendelea kumshukuru Mungu kwa jinsi tulivyoshuhudia vipawa mbalimbali vya watoto walivyonavyo na kufuta ile dhana ya kuwaona kama ni aibu katika familia na kuwafungia ndani kuwanyima haki zao za msingi ”Alisema Mch.Nkya.
Aidha alisema wamekuwa na siku hiyo maalumu kusisitiza umuhimi wa michezo kwa watoto na hasa makundi haya maalumu na kuinua vipawa vya watoto hao.” Michezo hii inalengo la kuchochea vipawa kwa vijana na kutambua kuwa Mungu anawapenda na jamii vile vile inawapenda na kutambua vipawa walivyo navyo”Alieleza Nkya.
Mratibu wa Kitengo cha Building a Caring Community (BCC), Mch. Anna Makyao alisema kwa kwa sasa wana jumla ya watoto 216 wanao wahudumia katika vituo na majumbani. Amesema BCC imeendelea kuwasaidi watoto kuhakikisha wanapata huduma za afya ikiwa ni pamoja na kuwapatia bima ya afya.
Amesema Pamoja na jitihada wanazofanya za kutembelea sharika kutafuta marafiki watakaowaunga mkono kwa michango ya aina mbalimbali kuweza kuwahudumia wahitaji hao, alitoa wito kwa jamii kuona haja ya kusaidia makundi maalumu ambayo yanaishi katika mazingira magumu.
Mratibu wa huduma kwa Watoto na vijana wenye ulemavu wa akili BCC, Bibi. Jescka Kileo amesema wameanda michezo kwa watoto hao kuwapa fursa ya kushiriki katika michezo kutokana na kundi hilo kusahaulika katika Nyanja za michezo.
“Tumeaandaa michezo hii kuwapa fursa watoto na vijana wenye ulemavu na wao kujifeel kama watoto wengine wanavyopewa nafasi ya kushiriki especially kwenye michezo”Alisema Bibi.Jescka.
Anasema licha ya kuwa na siku hii maalumu kwa ajili ya michezo, kila wiki siku ya Ijumaa wanakuwa na programu ya michezo kwa lengo la kuwasaidia kuimarisha afya ya akili na vilevile kuimarisha viungo vyao.
Anasema kila Ijumaa watoto na Vijana wanacheza mpira wa miguu, Parashuti, wanakimbia na kucheza ngoma. Anasema michezo mingine wanaocheza ni pamoja na kuruka kamba, kuvuta kamba, kujaza puzzle na michezo mingine kama kubembea na kucheza muziki.
Bulding a Caring Community BCC ni huduma inayoshughulika na watoto wenye ulemavu wa akili inayoshughulika na watoto waliopo nyumbani na wale waliopo kwenye vituo katika sharika 8 za manispaa ya Moshi. Katika sharika hizo kuna vituo ambayo vinawatunza watoto hao kuanzia asubuhi hadi jioni wanaporudi nyumbani.
BCC Ilianzishwa kutoa huduma hiyo kwa lengo la kuwasaidia katika matibabu, mazoezi ya mwili na pia kuwasaidia wazazi waweze kupata muda wa kufanya shughuli kutokana na kushindwa kufanya kazi wakiwa wanawahudumia watoto wao.