BCC Yapiga Hatua Zaidi

Mnamo Februari 25, 2024 Askofu Dkt. Fredrick Shoo Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini akishirikiana na Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya, Mkuu wa Jimbo la Hai Mch. Biniel Malyo na Mchungaji kiongozi wa Usharika wa Kingereka Mch. Crayson Munisi, aliongoza ibada rasmi ya uzinduzi wa huduma ya Bulding A Caring Community (BCC) ya kuwahudumia watoto na vijana wenye ulemavu wa akili katika Jimbo la Hai Usharika wa Kingereka.

Awali huduma hiyo ilikuwa ikitolewa katika baadhi ya Sharika za manispaa ya Moshi mjini, ambapo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007 hadi leo inatoa huduma kwa watoto zaidi ya 200 katika sharika 8 zenye vituo 11.

Ni katika kutimiza dhamira yao ya kutoa huduma katika sehemu mbalimbali hapa nchini, hatimaye Februari 25, 2024 wamepanua wigo kutoka manispaa ya moshi na kuanzisha huduma hiyo katika Jimbo la hai wakiandikisha jumla ya watoto 46 hadi sasa.

Katika ibada hiyo Askofu Dkt. Shoo mbali na uzinduzi wa huduma hiyo, pia aliweka jiwe la pembe nyumba ya ibada ya mtaa wa Sayuni, jengo la watoto wa BCC na kufungua nyumba ya ibada ya watoto wa shule ya jumapili. Kadhalika aliwastaafisha kwa heshima walimu 5 wa Elimu ya Afya ya Msingi jimbo la Hai.

Akihubiri katika Ibada hiyo, Askofu Dkt. Shoo aliwataka wakristo kuacha kuendekeza matendo maovu yaliyopo ndani ya mioyo yao na akili zao kwani mawazo maovu ndani ya Mkristo yanasababisha kuwatendea watu matendo mabaya ya kikatili.

Alisema kuwa ni vyema kila anayeona mawazo mabaya yanamwingia ndani yake kukataa mara moja kwani wanapoendekeza watajikuta wanatenda matendo ambayo watakuja kuyajutia katika maisha yao.

Askofu Dkt. Fredrick Shoo akitoa baraka wakati wa kuweka jiwe la msingi nyumba ya watoto wanaohudumiwa na BCC Usharika wa Kingereka Jimbo la Hai Februari 25, 2025