Katika kuadhimisha wiki ya Huduma kwa Wateja, Benki ya Uchumi imeweka wazi mpango wake wa kwenda mbele zaidi ya kawaida, kwa lengo la kuhakikisha wateja wanapata huduma bora zaidi ya matarajio yao.
Mpango huo umeelezwa na Happiness Daniel, Afisa Masoko wa Benki ya Uchumi, wakati akizungumza katika tafrija ya uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja iliyofanyika Oktoba 5, 2026, katika Tawi la Moshi Mjini.
Happiness amesema, wajibu wa Benki ya Uchumi hauishii katika kumpa mteja huduma za kifedha pekee, bali pia kuhakikisha anapata elimu ya fedha kwa ujumla, ikiwemo kumshauri aina ya akaunti inayofaa kulingana na malengo yake ya kifedha.
“Ni ahadi yetu kama Benki ya Uchumi kwenda mbali zaidi, yaani ‘Extra Mile’, ili kuhakikisha huduma ya fedha ambayo mteja anaipata inamsaidia kutimiza malengo yake,” amesema Bi. Happiness.
Licha ya kuadhimisha Wiki ya Huduma kwa Wateja, Happiness amesema Benki ya Uchumi imejipanga kutumia wiki hiyo kusikiliza maoni ya wateja kuhusu huduma zinazotolewa na benki hiyo.
“Tunatumia wiki hii kupokea maoni mbalimbali. Je, huduma hizi zinawaridhisha wateja kwa kiwango gani? Na kama hajaridhika na huduma, tunaangalia yale maeneo ambayo hatukufanya vizuri ili tuweze kuyafanya vizuri,” amesema.
Kwa upande wake, Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya Uchumi, Bw. Cornell Meseeck, amesema mteja ndiye uhai wa benki hiyo, akieleza kuwa bila mteja hakuna mafanikio katika benki.
Sambamba na hilo, Meseeck amewashukuru wateja kwa kuhudhuria uzinduzi wa Wiki ya Huduma kwa Wateja.
Aidha, Grace Komba, mteja wa Benki ya Uchumi kutoka Kata ya Majengo, Moshi, amepongeza huduma kwa wateja inayotolewa na benki hiyo pamoja na namna wateja wanavyothaminiwa.
Grace pia ameeleza namna mikopo yenye riba nafuu kwa vikundi vya wafanyabiashara inavyowanufaisha.
Naye Godwin Kakuru, ambaye pia ni mteja wa hiyo, amesema amenufaika na huduma za Benki ya Uchumi kwa zaidi ya miaka 10 na bado anaendelea kufurahia huduma anazopewa.
Wiki ya Huduma kwa Wateja huadhimishwa na taasisi mbalimbali duniani, huku Benki ya Uchumi ikitumia fursa ya wiki hiyo kuendelea kusikiliza wateja na kupata maoni yao kwa ajili ya kuboresha huduma.






