JUMA LA PENTEKOSTE- KARATU

Juma la Pentekoste lafunguliwa Karatu, zaidi ya wahubiri 164 na wapiga tarumbeta 80 washiriki!

Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mch. Deogratius Msanya, ameongoza ibada ya ufunguzi wa Juma la Pentekoste Usharika wa Karatu Mjini Mei 11, 2024.
Juma hilo Kidayosisi linafanyikia katika Jimbo la Karatu kuanzia Mei 11 – 19, 2024.

Msaidizi wa Askofu aliongoza ibada hiyo akishirikiana na Wakuu wa Majimbo ya Karatu {Mch. Barikiel Panga}, Siha {Mch. Elisa Kileo} na Hai {Mch. Biniel Mallyo}.

Wengine walioshiriki katika ibada hiyo ni Katibu wa Idara ya Elimu ya Kikristo {Mch. Fadhili J. Kiwera}, Wasaidizi wa Wakuu wa Majimbo ya Karatu {Mch. Phanuel Sippu} na Hai {Mch. Dominic Mushi}.

Juma la Pentekoste hufanyika kila mwaka kuanzia Juma la Exaud {Sikia kuomba kwangu} na kuishia Juma la Pentekoste {Kushuka kwa Roho Mtakatifu} katika kalenda ya Kanisa.

Katika Juma hili takribani Wahubiri zaidi ya 164 {Wachungaji 42, Wainjilisti 42, Wahubiri huru 80} watahubiri na kufundisha katika semina na mikutano ya Injili kwenye sharika 15 za Jimbo zenye mitaa 82.

Aidha, Wahubiri hawa wataambatana na Wapuliza tarumbeta 80 ambao Watahubiri kwa njia ya Tarumbeta kwenye sharika zote 15 za Jimbo la Karatu.

Baada ya kutangaza ufunguzi kwa niaba ya Mkuu wa Dayosisi, Mhe. Msaidizi Askofu Mch. Deogratius Msanya alitoa neno la utume na kuwatuma Wahubiri kutawanyika katika vituo 82 vilivyopangwa kwa ajili ya Juma la Pentekoste.

Juma la Pentekoste linatarajiwa kufungwa tarehe 19/05/2024 na Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mhe. Baba Askofu Dkt. Fredrick O. Shoo.