KINANDA CHA ZAIDI YA MILIONI 260 CHAZINDULIWA KANISA KUU MOSHI

Kinanda cha zaidi ya shilingi milioni 260 kimezinduliwa katika Kanisa Kuu la KKKT Moshi Mjini, Dayosisi ya Kaskazini Mei 23, 2021. Uzinduzi huo umefanywa na Mkuu wa KKKT na Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo.

Akisoma risala wakati wa uzinduzi huo Mch. Leonsi Shirima anayehudumu katika Kanisa Kuu la Moshi Mjini, alisema kinanda hicho kimechukua miaka miwili kukamilika na kimegharimu shilingi milioni 264 za Kitanzania.

Awali alimpongeza Askofu Dkt. Fredrick Shoo kwa kutoa wazo la ununuzi wa kinanda hicho mwaka 2018 na wazo hilo kupokelewa na washarika wa Moshi mjini. “Namshukuru Mungu kwa kutuwezesha kutimiza wazo la kununua kinanda cha kisasa lililotolewa na Baba Askofu Dkt. Shoo na kupokelewa na washarika kwa moyo na kuchangia kiasi hicho cha fedha.”Alisema Mch. Shirima.

Akizindua kinanda hicho, Mkuu wa Kanisa Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo alikipongeza Chuo cha Ufundi Hai chini ya Mkuu wa mafunzo Bw. Reinner Kammleiter, kwa kufanikisha utengenezaji wa kinanda hicho.

Alitoa wito kwa washarika wenye ujuzi wa kupiga kinanda kujifunza zaidi kuhakikisha kinanda hicho kinatumika kwa ukamilifu wote. Chuo cha Ufundi Hai (Hai Vocational Training Centre) kina karakana ya kisasa ya kutengeneza vinanda vya mbao (Pipe Organs), gitaa za galatoni na samani mbalimbali za mbao.Chuo kinamilikiwa na KKKT Dayosisi ya Kaskazini.

Mwalimu wa muziki kutoka Chuo Kikuu cha Makumira- Arusha, Bwana Randall Stubbs akipiga kinanda mara baada ya uzinduzi Mei 23, 2021 Kanisa Kuu Moshi Mjini