Maandamano ya Amani ya Vijana kuhimiza Kilimo Biashara.

Shirika la misaada la Norwegian Church Aid (NCA) kwa kushirikiana na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini wameongoza maandamano ya amani ya vijana kuwahamasisha vijana kushiriki katika Kilimo cha Biashara kuweza kujikwamua kiuchumi.

Maandamano hayo yaliyofanyika Agosti 04, 2022 yalianzia katika Makao Makuu ya Dayosisi ya Kaskazini Moshi Mjini na kuhitimishwa Lutheran Uhuru Hotel & Conference Centre ambapo Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa Dkt. Jairy Khanga (akimwakilisha Katibu Tawala) na viongozi wa dini mbalimbali walipokea maandamano hayo.

Maandamano hayo yaliyoambatana na semina kuhusu masuala ya kilimo yalianza katika mkoa wa Manyara na yatamalizika katika Mkoa wa kigoma yamelenga kuhamasisha vijana kujihusisha na shughuli za kilimo cha biashara na vilevile kuadhimisha miaka 75 tangu NCA ianzishwe.

Akizungumza katika semina hiyo msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Mch. Deogratius Msanya amewataka vijana na jamii kutumia uwezo Mungu aliowapa kutatua changamoto mbalimbali katika jamii hususani ukosefu wa ajira.

Amesema tunapaswa kukaa kwa pamoja kutatua changamoto zetu hasa ajira badala ya  kutafuta wa  kulaumiwa. “Tukae pamoja tutumie maarifa Mungu aliyotupa kufikiri na kutafuta namna ya kutatua changamoto ya ajira na sio kutafuta nani wa kupewa lawama”. Alisema Mchungaji Msanya.

Aidha alilipongeza shirika la NCA kwa kushirikiana na Kanisa kuwawezesha vijana na jamii kutengeneza ajira kwa njia ya Kilimo, ufugaji n.k.

Pia alitoa wito kwa vijana hao kuwa, watakapopata maarifa wanayofundiswha wawasaidie na vijana wengine amabao wanakata tamaa kwa sababu ya changamoto za ajira na uchumi jambo linalowapelekea kujihusisha na matendo maovu kama ujambazi.

“Kupitia programu hii tunapopata haya maarifa na kuyatekeleza tuwasaidie na vijana wengine. Hii itasaidia kuwaokoa kujihusisha na vitendo vya kihalifu vinavyoweza hata kupoteza amani yetu”. Alisema Mch. Msanya.

Mkurugenzi Mkazi wa shirika la Norwegian Chuch Aid (NCA) Tanzania, Mch. Berte Marie amesema shirika hilo limetimiza miaka 75 tangu kuanzishwa kwake na wameendelea kutimiza  lengo lao la  kutoa misaada mbalimbali duniani. Anasema licha ya misaada ya kiuchumi wanayotoa pia wanasaidia kuhakikisha watu wanapata haki.

Aidha alsema  wameanzisha vikundi vya ufuatiliaji na usimamizi wa miradi inayoanzishwa, vikundi vya miradi ya Kilimo, ufugaji nk.

Mch. Marie anasema katika kuazimisha miaka 75 ya NCA wametumia fursa hiyo kuwahamasisha vijana kujihusisha na shughuli za kilimo cha biashara. Tuendelee kukumbushana ushirikiano kuhakikisha maisha ya watoto wetu na jamii yanabadilika na kuwa bora zaidi.

Naye mgeni rasmi katika maandamano na semina hiyo kaimu katibu tawala wa mkoa Dkt. Jairy Khanga(Mwakilishi wa Katibu Tawala wa Mkoa) amepongeza ushirikiano uliopo kati ya serikali na dini. Anasema umeleta tija katika maendelo katika Nyanja mbalimbali kama elimu, afya, makundi maalumu na huduma nyingine nyingi za kijamii.

Anasema Tanzania ina fursa ya kukuza biashara za ndani na nje hususani katika masuala ya Kilimo.

“Mkoa wa Kilimanjaro umejipanga kuwawezesha vijana kushiriki katika sekta ya Kilimo;  Pongezi kwa Kanisa kuwezesha matembezi haya ya kuwahamasisha vijana kushiriki katika Kilimo biashara katika mikoa ya Manyara, Kilimanjaro na Kigoma.

Anasem serekali ipo tayari na itaendeleza ushirikiano na taasisi nyingine kuelekeza jitihada katika kutatua changamoto zinazosababisha vijana kuacha kujihusisha na suala la Kilimo.