Mch. Lyamuya Astaafu Kwa Heshima

Mkuu wa KKKT na Dayosisi ya Kaskazini Baba Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, ameongoza ibada ya kumstaafisha kwa heshima Mch. David Lyamuya Januari 8, 2023 katika Usharika wa Himo Jimbo la Kilimanjaro Mashariki.

Mch. David Lyamuya ametumika katika huduma ya kichungaji kwa miaka 30 na kama mwalimu kwa miaka 11. Akisoma wasifu wa Mchungaji Lyamuya, Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Mhandisi Zebadiah Moshi alisema Mch. alisoma shahada ya Theologia katika Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira mwaka 1987-1992. Vile vile alisoma shahada ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira mwaka 2001-2003.

Katibu Mkuu alisema mara maada ya kuhitimu shahada ya Thelogia mwaka 1992, alibarikiwa kuwa Mchungaji katika Usharika wa Mawanjeni Disemba 6, 1992.

Alitumika kama mchungaji kiongozi katika sharika za Kisamo (1992-1993), Mwika Kati(1994-1995) na mwaka 2007alitumika katika Usharika wa Kotela.

Vile vile Mch. Lyamuya alitumika kama Mkufunzi katika Chuo cha Biblia na Theologia Mwika mwaka 1995-2004, Chaplin katika Chuo cha Uongozi Masoka mwaka 2005-2006. Mwaka 2006 hadi Januari 8, 2023 alipostaafu kwa heshima alikuwa Chaplin katika Chuo cha Kumbukumbu cha Stefano Moshi (SMMUCo)

Aidha, Baba Askofu Dkt. Shoo alimpongeza kwa kutumia vipawa vyake kwa uaminifu katika kumtumikia Mungu. Aliwashukuru Washarika wa Himo kwa kazi kubwa waliyofanya ya kumstaafisha Mch. Lyamuya.

Katika somo la mahubiri lililohusu ubatizo, Mhe. Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya alisema katika ubatizo tunapaswa kuzingatia suala la ukiri wa imani na ahadi ya ubatizo. Alisema mara nyingi wakati wa ubatizo baadhi ya wadhamini wanakiri Imani na ahadi ya ubatizo kwa kusua sua.

“Tumekuwa tukizingatia zaidi hoja za Kitheologia kuhusu ubatizo wakati baadhi ya Wakristo wanashindwa kukiri Imani na ahadi ya Ubatizo kwa usahihi, na kuchambua maana yake.” Alisema Mch. Msanya

Alisema ahadi ya ubatizo ina mambo mawili, moja kumkataa shetani na mambo yake yote na kazi zake zote. Alisema watu wengi wanamkataa shetani kwa maneno na si kwa matendo.

“Mara nyingi hasa kipindi cha Krismasi wanakuja wakristo na kusema ahadi ya ubatizo kwa niaba ya watoto na Mchungaji anapotangaza wenye ndoa wabaki wanaondoka; nilikuwa kwenye mtaa mmoja siutaji jina waliondoka wote, Je, hatuoni hiyo contradiction ya wazi? Kumbe shetani huyo huyo unamkataa wakati huo huo umemkumbatia na ndiyo maana walipoambiwa wabaki wakaondoka hapo maana yake wanasema we Mchungaji kama unataka kutubariki we baki na Baraka yako sisi tuna rudi kuendelea na maisha yetu”.Alisema Mch. Msanya.

Alisema tunapaswa kujiuliza kama kweli tunaiishi ahadi ya ubatizo tuliyoikiri au inakuwa ni nadharia tu.

Sehemu yapili alisema ina mambo matatu moja, Najitoa kuwa wako. Anasema Ukristo ni kujitoa kwa ukamilifu kwa Kristo . Pili ni kutegemea, hii maana yake ni pale ambapo tumeweka tumaini letu nyakati za shida na mateso. Ukitikiswa ukaanza kuhangaika huku na kule maana yake hujaweka tegemeo lako kwa Mungu. “Wakristo nawaomba muweke tumaini lenu kwa Mungu”Alisistiza Mch. Msanya.

Aliongeza kuwa, Biblia inasema katika kitabu cha Yeremia 17:5.. ‘BWANA asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha BWANA’.

Na tatu alisema ni kutumika, hii maana yake ni kumtumikia Mungu popote pale Mungu alipo kuweka . “Tumika kwa uaminifu uwe daktari, mwalimu n.k tumika kwa uaminifu na Mungu atakutukuza, haya maneno yapo kwenye kitabu cha Warumi sura ya nane”.Alisema Mch. Msanya.

Alihitimisha kwa kuwasihi jamii na Wakristo kufanya kazi ya Bwana kwa uaminifu kwa maana Mungu atawapa thawabu.

Mch. David Lyamuya Aliyesimama mbele akistaafishwa kwa heshima na Mkuu wa KKKT na Dayosisi ya Kaskzini Askofu Dkt. Fredrick Shoo (mwenye kofia), Januari 8,2023 Usharika wa Himo