MKUTANO MKUU JIMBO LA KILIMANJARO KATI WAFANYIKA

Jimbo la Kilimanjaro Kati la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini, limefanya Mkutano wake Mkuu wa 15 Agosti 15, 2021 katika ukumbi wa Lutheran Uhuru Hotel& Conference Centre ambapo taarifa ya jimbo hutolewa na Mkuu wa Jimbo na kujadiliwa na wajumbe toka sharika zote za Jimbo kisha kuweka maazimio na mipango mbalimbali ya jimbo.

Mkutano huu hufanyika kila baada ya miaka miwili kwa mujibu wa Katiba ya Dayosisi ya Kaskazini ambacho ndicho chombo muhimu kinachotoa fursa ya kufanya tathimini ya utekelezaji wa mipango ya jimbo kwa miaka miwili iliyopita na kuweka mipango itakayofanyika ktika kipindi kingine cha miaka miwili.

Akisoma taarifa yake kwa Mkutano Mkuu wa 15 wa jimbo hilo, Mkuu wa Jimbo Mch. Javason Mrema  alisema Mkutano wanoufanya unaumuhimu mkubwa kwa mustakabali wa maendeleo na shughuli za jimbo kwani mipango na maamuzi yote ya jimbo hufanyika.

Alisema ni muhimu kwa wajumbe waliopata fursa ya kushiriki kutambua kuwa washarika wote wa jimbo zima wanategemea uwakilishi wao kikamilifu hasa katika kujadili na kuweka maazimio yenye tija na nayayotekelezeka kwa mustakabali wa maendeleo ya jimbo na Kanisa kwa ujumla.

Mch. Mrema alisema katika kuhakikisha wanaongeza ufanisi katika kutekeleza mipango na majukumu ya jimbo, wameandaa mpango Mkakati wa miaka kumi(2021-2030) wenye vipaumbele saba kama vilivyo katika Mpango Mkakati wa Dayosisi wa mwaka 2018-2022.

Alivitaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na: Kulea na kuimarisha maisha ya kiroho na Imani kwa washarika, kutoa huduma za Elimu na Afya zinazokidhi viwango bora na kuimarisha uongozi bora na uadilifu.

Vingine alivitaja ni pamoja na Kuimarisha uwajibikaji, kujituma na kujitolea katika kazi, Kujenga uwezo wa uendelezaji, usimamizi, ukusanyaji na mgawanyo wa raslimali katika jimbo, Kuboresha maisha ya washarika, vijana, watoto mambo ya jinsia na wasio na fursa na Kusimamia na kushiriki shughuli za bioanuai na mazingira.

Akinukuu neno Kuu kutoka kitabu cha Yohana 15:16a “Sii ninyi mlionichagua mimi, bali ni mimi niliyewachagua ninyi; nami ninawaweka mwende mkazae matunda;na matunda yenu yapate kukaa..” aliwataka wajumbe na Wakristo kutambua kuwa sio wao waliomuita Bwana bali ni Bwana aliyewachagua katika utume mkuu akawaaweka shamani mwake ili kumzalia Bwana matunda na matunda yapate kukaa.

Aliwata kumwomba Mungu awape Neema waweze kutimiza mapenzi yake katika kumtumikia na kumzalia matunda mema.

Baba Askofu Dkt. F. Shoo akifungua Mkutano Mkuu wa Jimbo la K/Kati

Mkutano huo ulizinduliwa na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania na Mkuu  wa Dayosisi ya Kaskazini ambye ndiye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Makanisa ya Kikristo Tanzania (CCT) Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo.

Jimbo la Kilimanjaro Kati

Jimbo la Kilimanjaro Kati ni mojawapo ya Majimbo Matano ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini lililoanzishwa mwaka 1982 kwa kugawanywa kutoka Jimbo la Kilimanjaro Mashariki. Wakati huo jimbo lilikuwa na idadi ya Sharika 12 na limekuwa na kufikia sharika 34 hadi sasa lina jumla ya Washarika Zaidi ya elfu 50 kwa takwimu za mwaka 2020.