Mkutano Mkuu wa 31 Wafanyika Jimbo la K/Mashariki

Mkutano Mkuu wa 31 wa Jimbo la Kilimanjaro Mashariki umefanyika Agosti 16, 2023 katika ukumbi wa Jimbo ambapo ulifunguliwa rasmi na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania na Dayosisi ya Kaskazini, Askofu Dkt. Fredrick Oanel Shoo. Katika mkutano huo taarifa ya jimbo hutolewa na Mkuu wa Jimbo na kujadiliwa na wajumbe toka sharika zote za Jimbo kisha kuweka maazimio na mipango mbalimbali ya Jimbo

Akifundisha neno la Ufunguzi wa mkutano Askofu Dkt. Shoo alisema, jamii inapaswa kuishi maisha ya uadilifu na ya hekima siku zote ikimtanguliza Mungu kwa kila jambo.

Alisema kwa sasa watu wameamua kuacha kumcha Mungu kwa makusudi na kutokumsikiliza Roho Mtakatifu na badala yake wanategemea akili na nguvu zao wenyewe.

“Tunahaja ya kujifunza na kuendelea kufundisha kumfahamu na kumsikiliza Roho mtakatifu, kumwamini na kumtii ili watu waweze kutambua kwamba Roho mtakatifu anatusaidia kupambanua, hata kupambanua roho zidanganyazo na mafundisho potofu; Bila roho mtakatifu tutakuwa tunaangamia”.Alisema Askofu Dkt. Shoo

Alisema hatuwezi kuenenda kama watu wenye hekima kama hatutamtanguliza Roho Mtakatifu katika maisha yetu. Bwana Yesu anatufundisha ili tuweze kuifahamu kweli ya neno la Mungu ni sharti kumtanguliza Roho mtakatifu.

Naye Mch. Gudluck Kitomari alifundisha neno kuu kutoka kitabu cha Hosea 4:6a linalosema watu wangu wanaangamizwa kwa kukosa maarifa…

Alisema  Mungu anachukizwa na wanaofundisha mafundisho ya uwongo na vilevile kwa wale wafundishwao na kukosa maarifa ya kujua kweli ya Neno la Mungu.

“Tunahitaji Injili, tunahitaji kufundisha watu dhambi ni nini, wokovu ni nini maana watu wanatatanika na kupotoka kwa kutokufanamu.”Alisema Mch. Kitomari

Alisema Wachungaji wanapaswa kuwa wa kwanza kufahamu roho, kuzipima, kuwatahadharisha watu maana wanahitaji Elimu. Tusipowafundisha watu na kuwajengea misingi mizuri tutawapoteza.

“Tuwakumbushe watu kuwa wanakombolewa kwa Neema, ukombozi na kuwa katika wokovu kunapatikana kwa kumcha Mungu.”Alisema Mch. Kitomari

Akisoma taarifa ya Jimbo, Mkuu wa Jimbo la K/Mashariki ambaye ndiye mwenyekiti wa Mkutano Mch. Calvin Koola aliwashukuru na kuwapongeza wanajimbo kwa kutunza Umoja ndani ya Jimbo, Dayosisi na Kanisa.

Akizungumzia suala la mazingira aliwakumbusha Wachungaji Viongozi wa Sharika kusimamia agizo la Mkutano Mkuu wa Dayosisi la kuotesha miti 20 na kuitunza kabla ya mwanafunzi wa Kipaimara kubarikiwa ili kuendeleza dhamira ya Dayosisi, Kanisa na Taifa ya kutunza mazingira.