Mkutano Mkuu wa 5 wa Wachungaji wa KKKT wafanyika Dodoma

Mkutano Mkuu wa Wachungaji wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Unafanyika katika jiji la Dodoma kuanzia Septemba 10-15.

 Ibada ya ufunguzi ilifanyika Jumapili ya Septemba 11, 2022 katika Kanisa Kuu la Dayosisi ya Dodoma na iliongozwa na kaiumu Mkuu wa Kanisa Askofu Dkt. Alex Malasusa aliyemwakilisha Mkuu wa Kanisa Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo.

Takribani wachungaji 2000 wamehudhuria Mkutano huo na Neno kuu la Mkutano huo limetoka katika kitabu cha 1Pet 5:2 linalosema ‘Lichungeni kundi la Mungu’. Mkutano kama huu kwa mara ya mwisho ulifanyika mwaka 2016 ambao ulilenga mandalizi ya maadhimisho ya miaka 500 ya matengenezo ya Kanisa yaliyofanyika mwaka 2017.

Akifungua Mkutano huo wa tano kwa niaba ya Mkuu wa Kanisa Askofu Dkt Fredrick Onael Shoo, Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani Dkt Alex Malasusa ameiomba serikali kuwasaidia viongozi wa dini kudhibiti suala la vijana  kupenda zaidi kucheza michezo ya kubahatisha badala ya kufanya kazi.

Aidha Askofu Dkt Malasusa amesema  Kanisa linakabiliwa na changamoto ya mafundisho ya uongo walimu wa uongo na mapato ya hila yanayotumia jina la Yesu.
Amewaomba viongozi wa dini kuwasaidia katika hili kwani linasababishwa na kukosekana kwa hofu ya Mungu.

Katika mkutano huo Wachungaji watajadili mada mbalimbali zikiwamo umoja na utambulisho wa Kanisa na Katiba moja ya KKKT.