Nkweseko:Nyumba ya Mtumishi yafunguliwa

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania na Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini  ambaye ni mwenyekiti wa Jumuia ya Makanisa ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo amezindua nyumba ya Mtumishi ya Usharika wa Nkweseko Septemba 2, 2021 katika Usharika wa Nkweseko.

Nyumba hiyo hadi kukamilika imegharimu kiasi cha zaidi ya shilingi milioni 90 za Kitanzania ikiwa ni michango ya Washarika wa Nkweseko waliopo usharikani na wale walio safarini.

Akizindua nyumba hiyo Mkuu wa Kanisa Baba Askofu Dkt. Shoo aliwapongeza washarika wa Nkweseko kwa kuoana umuhimu wa kujenga nyumba ya Mchungaji itakayomsaidia apate mahali pa kuishi akifanya kazi ya Mungu.

Katika pongezi zake alisema washarika wameamua kujenga nyumba hiyo kama ishara kuwa wanamhitaji Mchungaji akae katikati yao akiwahudumia “Kujenga nyumba hii ni ishara kuwa Washarika wa Nkweseko wanataka mchungaji uwe katikati yao ukiwahudi, mchungaji hongera na uende ukawahudumie watu wa Mungu, watembelee wagonjwa, wazee na kuwaombea  watu wa Mungu Baraka” alisema Dkt. Shoo Akisoma neno la Mungu kutoka kitabu cha Mhubiri 9:10 “Lolote mkono wako utakalopata kulifanya, ulifanye kwa nguvu zako; kwa kuwa hakuna kazi, wala shauri wala maarifa, wala hekima, huko kuzimu uendako” nakusema kuwa neno hilo ndilo walililolifanya na kuwapa washarika wa Nkweseko nguvu na hari ya kufanya kazi zao kwa moyo na kwa upendo.