Sembeti: Askofu Dkt. Shoo Aongoza Ibada ya Uzinduzi Nyumba ya Mchungaji, Darasa la Chekechea na Ofisi

Mkuu wa KKKT na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, amefungua nyumba ya Mchungaji wa Usharika wa Lembeti, Darasa la Chekechea, Ukumbi wa Mikutano wa Usharika pamoja na kuweka wakfu Mimbara ya Usharika  Aprili 6, 2023.

Kwa mujibu wa Mchungaji kiongozi wa Usharka wa Sembeti Richard Njau, amesema majengo hayo yamejengwa kwa michango ya washarika walio ndani na walio safarini pamoja na marafiki.

Amesema Nyumba ya mchungaji imegharimu kiasi cha shilingi milioni 78 na darasa la chekechea shilingi milioni 18. Aidha kwa upande wa ofisi amesema imegharimu kiasi cha takribani milioni 7.  Alimshukuru Mkuu wa Kanisa kwa kukubali kuja kufungua majengo hayo

Akihubiri katika ibada hiyo ya Alhamisi Kuu, Baba Askofu Dkt. Shoo alisema Wakristo wanawajibu wa kutii agizo la Yesu la kushiriki Mwili na Damu ya Kristo. Anasema katika kushiriki meza ya Bwana kusifanywe kwa mazoea bali  kufanyike kwa  unyenyekevu mkubwa na kwa toba ya kweli.

“Unapaswa kujiandaa kiroho kuhusu dhambi zako, mwenendo wako, mahusiano yako na wanaokuzunguka kabla ya kushiriki meza ya Bwana”. Alisema Askofu Dkt. Shoo

Alisema Wakristo wanapaswa kujuta kuhusu dhambi zao, kutubu, na kuamini kweli tunapokea ondoleo la dhambia kwa kushiriki meza ya Bwana.

Alihitimisha kwa kusema Yesu alikufa ili sisi tupate kuhesabiwa haki na Kanisa limekuwa likitii agizo la Yesu la  kushiriki sakramenti na la ubatizo. Yesu mwenyewe aliwataka wanafunzi wake na wote wanaomwamini  kushiriki meza ya Bwana  kila wakati  huku wakikumbuka kuwa yeye mwenyewe aliutwaa mwili wake na kuimwaga damu yake pale msalabani.

Baba Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo mwenye fimbo kwenye picha ya Pamoja na wanafunzi wa Chekechea mara baada ya kufungua Darasa la Chekechea Usharika wa Sembeti Aprili 6, 2023