TUNAJALIZA, HATUSHINDANI NA SERIKALI

Mwenyekiti wa Kilimanjaro Interfaith, Mhe. Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, ameitaka Serikali itambue kwamba huduma za kijamii zinazotolewa na taasisi za kidini hazina lengo la kushindana na huduma za kijamii zinazotolewa na serikali. Lengo la taasisi za dini kutoa huduma za elimu na afya ni kujaliza pale penye upungufu katika kuisaidia serikali kutimiza majukumu yake katika kutoa huduma bora za elimu na afya nchini.

Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo akiwasilisha mada kuhusu bima ya afya kwa wote kwa kuzingatia lengo la 3 la umoja wa mataifa, ameitaka serikali kuelewa kwamba kuweka bajeti toshelevu isichukuliwe kama gharama bali uwekezaji katika maendeleo ya binadamu.

Aidha, ameitaka serikali kuwasilisha muswada wa sheria ya bima ya afya bungeni na itoe fursa kwa wadau kuujadili ili kufikia sheria nzuri itakayosimamia afya bora kwa wananchi wote bila ubaguzi.

Katika majadiliano ya mada hiyo, Mhe. Dkt. Anna Mghwira, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, alipendekeza kwamba iundwe kamati ndogo (Task-force) iwasilishe mapendekezo halisi yaliyotokana na utafiti kuhusu bima ya afya kwa wote kuwa  inawezekana.

Kongamano hilo la viongozi wa dini mbalimbali Mkoa wa Kilimanjaro lililofanyika tarehe 31 Mei, 2021 Uhuru Hotel & Conference Centre, walitumia fursa hiyo kumuaga kwa heshima Mhe. Dkt. Anna Mghwira na kumkaribisha Mkuu Mpya wa Mkoa Mhe. Stephen Kagaigai.

Baadhi ya viongozi wa Dini Mkoa wa Kilimanjaro, wakimkabidhi zawadi aliyekua Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro Dkt. Anna Mghwira aliyemaliza kipindi chake.