Viongozi Muwe Mfano Katika Utoaji

Askofu Mstaafu Dkt. Erasto N. Kweka wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, amewataka viongozi wa Kanisa kuwa mfano kwa waumini wao katika utoaji sadaka kwani waumini wanapoona kiongozi anajitoa na wao watakuwa na moyo wa kujitoa  kwa furaha na upendo.

Askofu Dkt. Kweka aliyasema hayo wakati akifundisha semina ya Uwakili kwa viongozi wa Sharika iliyofanyika katika Usharika wa Mwika Kati ukihusisha sharika za Jimbo la Kilimanjaro Mashariki kanda ya Mwika Kaskazini na Kusini Machi 15, 2023.

Alisema ili elimu ya uwakili ienee vizuri, viongozi wanapaswa kuwa mfano bora wa kuigwa; Mchungaji au kiongozi wa kikristo hawezi kuepuka wajibu wake wakujitolea sehemu yake ya mali kwa Mungu na kwa kufanya hivi usharika utapata baraka nyingi kwa Mungu.

“Watumishi wanapaswa kuwa mfano wa kutoa sadaka   kwa upendo na katika kutoa kuna Neema ya Mungu na pia kunakuwa na Baraka za Mungu  kwenye maisha yao; ni vyema kutoa sadaka bila ya kujilinganisha na mtu awayae yote” Alisema Askofu Dkt. Kweka.

Akifafanua maana ya uwakili alisema kuwa uwakili ni kukabidhiwa madaraka juu ya maisha, miili yetu, muda, uwezo, karama, mali na injili ili kuvitunza na kuvitumia kufuatana na matakwa ya aliyevitoa ambaye ni Mungu.

Alisema Uwakili unahusu mambo muhimu 3, moja mtoaji amana au mali ambaye ni Mungu, pili mkabidhiwa ambaye ni mwanadamu  na tatu ni mali yenyewe.

“Kwahiyo uwakili ni hali nzima ya kupokea amana na kutumia amana na mwisho wa siku tunatakiwa kutoa hesabu ya amana tulizopewa na mwandishi wa agano la kale anasema Mungu ndiye liyetupa vitu  hivyo vyote’’Alisema Askofu Kweka

Naye Katibu wa Idara ya Uwakili na Mipango ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mch. Andrew Munisi alisema kuwa, semina hii ilianza toka mwaka jana kwenye baadhi ya majimbo na itaendelea kutolewa.

Viongozi mbalimbali katika sharika wakifuatilia somo la Uwakili lililofundishwa na. Baba Askofu Dkt. Kweka, Machi 15, 2023