“Viongozi tutende kulingana na nyakati, miaka ishirini iliyopita tuliweza kusema hapana wanafunzi wametosha. Je, bado tunaweza kusema hivyo sasa?”

“Viongozi tutende kulingana na nyakati, miaka ishirini iliyopita tuliweza kusema hapana wanafunzi wametosha. Je, bado tunaweza kusema hivyo sasa?”

Msd. Ask. Mch. Dogratius Msanya aliyasema hayo wakati akifungua Warsha ya Wakuu wa Shule, Walimu wa taaluma na Wenyeviti wa Bodi za Shule za Sekondari za Dayosisi iliyofanyika Alhamisi tarehe 8 Disemba, 2022 Lutheran Uhuru Hotel and Conference Centre iliyopo Shanty.

 “Ni muhimu kuzingatia kwamba, wakati wengine tunakuna vichwa kufunga shule, wengine wanaona fursa ya uwekezaji katika huduma ya elimu. Ni muhimu na lazima kujiuliza tena, tunakwama wapi? tunaweza kufanya nini kimkakati zaidi?” aliendelea kusema Msd. Ask. Mch. Msanya. Kisha alitoa kongole na shukurani kwa Wenyeviti wa Bodi ambao wameonesha moyo wa kujituma na kujitolea kwa dhati katika kusimamia uendeshaji wa shule za sekondari za Dayosisi kwani ni watu wenye majukumu binafsi n.k.

Naye Mudiri wa Elimu wa Dayosisi Dkt. Estomi Makyara aliwakaribisha na kuwatambulisha washiriki na wa wezeshaji  akisisitiza kwamba, lengo kuu la warsha hii ni kujengewa uwezo katika Kufikiri Kimkakati ili kupiga hatua kutoka hapa tulipo na kwenda mbele zaidi.

Mada zilizowasilishwa ni pamoja na  Muundo wa Elimu ya Sekondari  iliyowasilishwa na Ndg. Joshua Moshi kutoka  Christian Social Services Commission (CSSC) akisisitiza kwamba, ni wajibu wa kila mjumbe wa bodi ama kamati za bodi kuifahamu kwa kina Sera ya Elimu ya Taifa sambamba na Sera ya Elimu ya Dayosisi. Aidha, alilisisiza umuhimu na ulazima wa ugatuzi unaozingatia sheria na kanuni na si kiongozi fulani kuwa ndiye shule na shule ndiyo yeye. Alihitimisha mada yake kwa kuhimiza umuhimu wa kuwa na utambulisho wa shule za Kanisa.

Naye Prof. Declare Mushi katika mada yake ya Wajibu, Sifa na Mipaka ya Bodi alisisitiza kwamba, kuna aina kadhaa za tabia au utendaji wa bodi k.v. bodi zinazokubali kila kitu, bodi zisizojali kila kitu, bodi zinazojihusisha na masuala fulani tu, bodi zinazojihusisha na kila suala. Aliwaasa washiriki kuhusu hali ya kufanya uamuzi wa mambo makubwa ilhali wana taarifa chache sana au kufanya uamuzi mdogo ilhali wana taarifa nyingi sana.

Mada ya mwisho iliwasilishwa na Ndg. Peter Kithyaka kuhusu Kufikiri Kimkakati aliyetaja kwamba, ni muhimu kila mara viongozi kuzingatia mambo muhimu manne (4) wanapofanya uamuzi. Mambo hayo ni pamoja na Uimara wetu, Udhaifu wetu, Changamoto zetu na Fursa zilizopo. Ndg. Peter Kithyaka aliwasisimua washiriki kwa kutaja kwamba, ikiwa shule A imezungukwa na shule B, C na D, n.k., shule A inapaswa kuziona shule hizo kuwa ni fursa kwake kwani kila wanakati wanafunzi huhitaji shule bora zaidi! Aidha, alishauri umuhimu wa kutumia njia mbalimbali katika kuhimiza uwajibikaji ikiwa ni pamoja na wanafunzi kuwapima walimu kila mwisho wa muhula kwa kutumia nyenzo maalumu.

Warsha ilihitimishwa saa 9 alasiri.


Picha ya pamoja Msd. Ask. Mch. Msanya D (katikati walioketi) akiwa na wawezeshaji waliokaa na waliosimama ni wenyeviti wa bodi za shule