Viongozi waingizwa kazini Longuo

Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Kati, Mch. Javason Nelson Mrema akiwasimika Wazee wa Kanisa Usharika wa Longuo Tarehe 14/03/2021

Ni Jumapili ya tarehe 14 mwezi Machi, 2021 katika Usharika wa Longuo Jimbo la Kilimanjaro Kati, karani wa Usharika Bi. Beatrice Kimaro aliingizwa kazini rasmi pamoja na wazee wapya wa Usharika.Tendo hilo lilienda sanjari na kuwaaga wazee wa Usharika waliomaliza kipindi chao cha uongozi kikatiba.

Tendo hilo la kuwaingiza wazee wapya kazini,kustaafisha na kumwingiza kazini karani wa Usharika lilifanywa na Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Kati Mchungaji Javason Mrema akishirikiana na Mchungaji kiongozi wa Usharika Richard Njau pamoja na Mchungaji mwenza  Tumaini Minja.

Katika Ibada hiyo Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Kati aliwataka Wakristo na jamii kufanya kazi kwa bidii huku  wakimtegemea Mungu kuweza kupata mahitaji yao ya kila siku.

Alitoa angalizo kwa baadhi ya watu wanaodhani kuwa na Imani bila kufanya kazi kwa bidii watafanikiwa katika maisha “Pamoja na kumtegemea Mungu lazima kufanya  kazi kwa juhudi kubwa kufikia mafanikio katika maisha, kutafuta maisha kwa bidii ili ufanikiwe si kukosa Imani bali ni kuiamini Imani yako kwa vitendo” Alisema Mch. Mrema.

Alisema  tunapaswa kufanya kazi kwa bidii na kumtegemea Mungu katika shughuli zetu”Tunakumbushwa kumtegemea Mungu katika kila jambo na Mungu hatatuacha kamwe.” Alisema Mch. Mrema.