“Wanawake na wanaume msipotelee kwenye kombe la Dunia.. na kama ilivyo mnavyotunza tiketi kuingia uwnjani kutizama mpira huko Qatar vivyohivyo Wakristo tutunze tiketi zetu za uzima wa milele yaani imani katika Yesu Kristo”

Hayo aliyasema Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, akihubiri katika Ibada ya kumstaafisha kwa heshima Mch.  Onesforo David Usiri iliyofanyia katika Usharika wa Mroma Jimbo la Hai Novemba 20, 2022.

“Msipotelee huko kwenye world cup ninyi wanawake na wanaume maana siku hizi hata wanawake ni ashabiki wazuri pia; kumbukeni pia kutunza tiketi zenu yaani imani katika Yesu ili muingie uzimani kama ambavyo mashabiki wanatunza tiketi za kuingia uwanjani kule Qatar” Alisema Askofu Dkt. Shoo.

Aliwakumbusha Wakristo kuwa, Yesu aliyezaliwa na kufa kwaajili ya zambi zetu na kisha akafufuka na kupaa Mbinguni atakuja kwa hukumu ya mwisho.

Askofu Dkt. Shoo alisema tusisahau wala kudanganyana kuwa hukumu ya mwisho haita kuwepo. Yesu ndiye atakayetoa hukumu hiyo na wale walio mwamini na kuvumilia mpaka mwisho wakitunza tiketi zao ndiyo watakaoshinda na kuungana pamoja na watakatifu wote wakikaa na kumsifu Mungu milele.

Naye Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini  mhandisi Zebhadia S. Moshi alishukuru na kutoa kongle kwa Jimbo la Hai na usharika wa Mroma kwa kuandaa ibada hiyo.  Pia almshukuru na kumpa kongle mke wa Mch, Usiri kwa kumtunza mume wake ambaye pamoja na umri wa kustaafu bado anaonekana kijana.

Naye Mch. Usiri katika neon la itikio lake alikumbuka jinsi wazazi wake walivyohusika katika kuchochea wito wake kwa kumshawishi kumtumikia Mungu katika huduma ya Kichungaji.

Mchungaji Usiri ametumika katika huduma ya Kichungaji kwa miaka 34. Alisoma Stashahada ya theologia mwaka 1983 hadi 1987 katika Chuo Kikuu cha Tumaini Makumira. Alibarikiwa kuwa Mchungaji mwaka 1988 katika Usharika wa Ngira na kuhudumu katika sharika mbaimbali ikiwa ni pamoja na Usharika wa Lawate, Fuka, Mungushi, Nronga na Nkwarungo.

Sharika nyingine alizohudumu ni  Kisirenyi, Nshara, Sawe, Nkwansira, Hai Mjini na kuanzia mwaka 2016 hadi kustaafu kwake alihudumu katika Usharika wa  Mroma.

Mch. Onesforo David Usiri Kulia akiwa na Mke wake siku ya Kustaafu kwake Usharika wa Mroma Novemba 20, 2022