Msaidizi wa Askofu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Mch. Deogratius Msanya, amewakaribisha wageni kutoka Sinodi ya Nebraska Marekani, wakiongozwa na Askofu Johnson Scott, waliotembelea Ofisi Kuu za Dayosisi ya Kaskazini, Septemba 1, 2026.
ELCA Sinodi ya Nebraska ni rafiki na mshirika wa muda na Dayosisi ya Kaskazini, huku mahusiano yao yakijengwa katika misingi ya urafiki, upendo na umoja katika Kristo.
Akizungumza mara baada ya utambulisho, Askofu Johson Scott wa Sinodi ya Nebraska amesema, amefurahi kushiriki pamoja na waumini na viongozi wa Dayosisi ya Kaskazini katika Sala ya Asubuhi.
Askofu Johnson amesema amefurahishwa kusikia kutoka kwa mhubiri wa siku hiyo kwamba mahusiano kati ya Dayosisi ya Kaskazini na Sinodi ya Nebraska si ya kimradi pekee, bali ni mahusiano ya kifamilia na kirafiki.
Amesema anakubaliana na mtazamo huo kwa kuwa mara kadhaa wanapokutana, hukutana kama marafiki na watu wanaounganishwa na huduma ya Kanisa, huku wakitambua kwamba wao ni kaka na dada katika Kristo, licha ya kuhudumu katika maeneo tofauti.
Aidha, amesema mahusiano hayo ni sehemu ya juhudi za kujenga mahusiano ya Kikristo duniani kote, jambo ambalo, kwa mujibu wake, linampa Mungu furaha na utukufu.
Awali, Katibu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Mhandisi Z. S. Moshi, akimkaribisha Msaidizi wa Askofu na ujumbe kutoka Sinodi ya Nebraska, amesema Dayosisi ya Kaskazini na Sinodi ya Nebraska zina mahusiano yaliyojengwa katika urafiki na upendo wa Yesu Kristo.
Baada ya utambulisho huu uliofanyika katika sala ya asubuhi, Askofu Scott na ujumbe wake wamefanya kikao na wakuu wa idara mbalimbali za Dayosisi ya Kaskazini ili kubadilishana uzoefu na uwasilishaji wa uelekeo wa urafiki baina ya Sinodi ya Nebraska na Dayosisi ya Kaskazini.



