• Mch. Blandina Astaafu kwa Heshima
  • Atumika Miaka 30 na…

Mkuu wa KKKT na Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, ameongoza ibada ya kumstaafisha kwa heshima Mch. Blandina Faustin Sawayael Shoo, baada ya kutumika kwa takribani miaka 30 na miezi 7. Ibada hiyo ilifanyika katika Usharika wa Karanga Jimbo la Kilimanjaro Kati la KKKT Dayosisi ya Kaskazini Julai 23, 2023.

Katika ibada hiyo Mhe. Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya alihubiri somo kutoka kitabu cha Matendo ya Mitume 6:1-6 lenye kichwa cha Uchaguzi wa Busara. Alisema katika somo tunajifunza jinsi ya kufanya uchaguzi wa busara kama wale wanafunzi waliotajwa katika somo jinsi walivyofanya uchaguzi wa Busara kwa kuona si vyema kuacha kazi waliyoitiwa ya kuhubiri Injili na kwenda kugawa vyakula badala yake walitumia busara kuteuwa watu wenye busara watakaogawa mahitaji na kunukuu maneno kutoka Matendo 1:2-4.

“Kwa hiyo, mitume kumi na wawili waliita jumuiya yote ya wanafunzi, wakasema, “Si vizuri sisi tuache kulihubiri neno la Mungu ili tushughulikie ugawaji wa mahitaji. Hivyo, ndugu zetu, chagueni miongoni mwenu watu saba wenye sifa njema, waliojawa na Roho na wenye hekima; nasi tutawakabidhi jukumu hilo. Sisi, lakini, tutashughulika na sala na kazi ya kuhubiri neno la Mungu.” Alinukuu maneno kutoka Matendo 1:2-4.

Mch. Msanya alisema ni jambo la busara kuchagua kwa kuzingatia  vipau mbele na  hata wale tunaowachagua katika kufanya kazi inafaa kuzingatia watu wenye busara, hekima, wenye kumcha Mungu  na kujawa na Roho Mtakatifu.

“Katika kutafuta viongiozi katika Kanisa, taasisi na kwingineko tunapaswa tutafute watu  wenye ushuhuda mzuri katika maisha yao ili wasijeleta makwazo kwa watu wanaowaongoza au kuwatumikia. Sisi Wakristo tunapaswa  kufanya uchaguzi wa kumchagua  Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo, awe nasisi siku zote za Maisha Yetu”.

Kabla ya tendo la kumstaafisha Mch. Blandina Shoo, Mhe. Katibu MKuu wa Dayosisi ya Kaskazini Mhandisi Zebadiah Moshi alisoma historia ya Maisha ya Utumishi ya   Mchungaji. Alisema Mch. Blandina Sawayael Shoo baada ya kumaliza masomo yake katika chuo Kikuu cha Makumira mwaka 1992; alibarikiwa kuwa Mchungaji Januari 3, 1993 katika Usharika wa Majengo.

Alisema mara baada ya kubarikiwa Mch. Blandina alihudumu katika sharika za Majengo (1993-1996) na Shiri (1996-197). Vilevile katika maisha yake ya utumishi alifanya kazi mbalimbali za kujitolea na alitumika katika mashirika mbalimbali kwa kazi za jamii.

Katika itikio lake Mch. Blandina alimshukuru Mungu kwa kumtia nguvu na kumvusha mahali ambapo hakuweza kwa nguvu zake katika kipindi cha utumishiwake. Vile vile alimshukuru Mkuu wa Kanisa  na Kanisa kwa  jinsi walivyomlea tangu alipopata wito wake na kumwombea katika utumishi wake hadi kufikia siku yake ya kustaafu.

Aliwahimiza vijana kujiunga na kuwa watumishi katika shamba la Bwana na vilevile  aliwataka wababa na wamama kushirikiana kwa pamoja katika kumtangaza Yesu Kristo.

Kuhusu wimbi la ukatili wa kijinsia, alitoa wito kwa washarika kuwatafuta wale wenye nyumba wasizozitumia ambao huenda wapo safarini kuona uwezekano wa kupata vituo ambavyo vitawasaidia watu wenye matatizo kama hayo ya ukatili kupata msaada kwa haraka. “Kuna Wanasheria, watu wa ustawi wanaoweza kuwasaidi wahanga wa ukatili, tuwape nafasi katika hizo nyumba”. Alisema Mch. Blandina.

Akihitimisha kwa kutoa salam za Kanisa Mkuu wa KKKT na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Shoo, alisema Mch. Blandina alitumika kwa uaminifu katika utumishi wake hasa katika miradi mfano Norwegian church Aid na hakuwa na upendeleo.

“Sisi tunakutakia baraka za Mungu Mungu akikushika mkono nawewe ukajikabidhi kwake utakuwa salama na hakuna litakaloshindikana kwako”. Alisema Dkt. Shoo

Alitoa wito kwa Wana KKKT kuendelea kuliombea  Kanisa ili Mungu azidi kulisimamisha Kanisa na kusimama imara katika kweli ya neno la Mungu.

“Tuliombee Kanisa maana kutakuwa na mkutano Mkuu wa KKKT ambapo pia kutakuwa na uchaguzi wa Mkuu mpya wa Kanisa ili apatikane ambaye atakuwa si kwa mapenzi ya wanadamu bali kwa mapenzi ya Mungu”.Alieleza Dkt. Shoo

Alisema tusipoomba kwa dhati, na tusipochagua kwa busara na hekima kwa kuongozwa na Roho wa Mungu tutakuwa na watumishi na viongozi wasio wa baraka katika jamii.

Aidha, alihitimisha kwa kulishukuru Jimbo la Kilimanjaro Kati, Ofisi ya Msaidizi wa Askofu, Usharika wa Karanga kwa kumstaafisha kwa heshima Mch. Blandina Faustin Sawayaeli Shoo.