Askofu Stubkjaer atembelea Ushirika wa Neema

Rais wa fungamano la makanisa ya Kilutheri Duniani Askofu Henrik Stubkjaer katika ziara yake alipata fursa ya kutembelea Kituo cha Masista wa Ushirika wa Neema.

Masista wa Ushirika wa Neema ni kituo chenye makao yake makuu mjini Moshi -Tanzania, ni jumuiya ya masista wa Kilutheri, ambayo inajishughulisha zaidi na masuala ya elimu na kilimo. Tangu mwaka 1994 wamekuwa wakitoa mafunzo kwa walimu wa chekechea katika kituo cha mafunzo cha Montessori mjini Moshi. Wahitimu wengi wa kituo hicho cha mafunzo wameajiriwa katika taasisi za Kilutheri. Masista hao wanaendesha shule mbili za chekechea za Montessori, kituo cha watoto yatima na shamba wenyewe. Pia wako katika harakati za kuanzisha shule ya msingi ya Montessori. Masista wa Ushirika wa Neema walianzishwa mwaka 1979 na watawa wa Augsburg. Sister Elistaha Mlay kwa sasa anasimamia masista takriban 69.