Rais wa LWF katika Ziara yake Nchini Tanzania

Rais wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani ( Lutheran World Federation-LWF) Askofu Henrik Stubkjaer amekuwepo nchini Tanzania kwa ziara ya siku 3 akitembelea Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT).

Ziara hii ni ya kwanza tangu kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa LWF mwezi Septemba, 2023 katika Mkutano wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani uliofanyika Krakow Poland ambapo amepokelewa na mwenyeji wake Mkuu wa KKKT Askofu Dkt. Alex Malasusa.

Askofu Stubkjaer ameambatana na ujumbe wake akiwemo Makamu wa Rais Kanda ya Afrika Mch. Dkt. Yonas Dibisa.

Katika ziara hiyo ametembelea Chuo Kikuu Cha Tumaini Makumira, Shirika la Msamaria mwema na tasisi zake ikiwemo Hospitali ya Kanda ya KCMC kuona namna Kanisa linavyoendesha shughuli zake kupitia taasisi zake.

Pia ametembelea ofisi Kuu ya Dayosisi ya Kaskazini, Bank ya Uchumi (UCB) pamoja na kituo cha Masista wa Ushirika wa Neema Moshi kuona jinsi ambavyo kanisa linaendesha taasisi zake. Alipokelewa na Mkuu wa Dayosisi ambaye ni Mkuu wa KKKT Mstaafu Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo.

Pia katika ziara hiyo atapata fursa ya kushiriki majadiliano kuhusu matumizi ya nishati Jadidifu (Renewable Energy) na viongozi mbalimbali wa dini na serikali.