Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Mashariki Mch. Calvin Koola ameongoza Ibada ya uzinduzi wa maadhumisho ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Sharika za Rombo, ambapo uzinduzi huo ulifanywa katika Usharika wa Rongai Agosti 20, 2023
Awali akihubiri katika ibada hiyo, Mch. Koola alimshukuru Mungu kwa sharika hizo kufikisha miaka 50 ukanda wa Rombo.
Mch. Koola alitoa rai kwa wachungaji na wainjilisti kuhubiri injili kwa watu na kufanya uinjilisti wa nyumba kwa nyumba ili Sharika zikue na kuzaliwa Sharika nyingine zaidi.
Kuzaliwa kwa Sharika za Rombo
Kwa mujibu wa Risala iliyosomwa na Mch. Mstaafu Dkt. Eliasi Silayo alisema nuru ya injili iliangazia eneo la Rombo kutoka Usharika wa Mwika kati ya mwaka 1954 chini ya uongozi wa Hayati Mch :Kalebi Mangesho. Mahali pa kwanza kabisa kufikiwa injili Rombo ni Mtaa wa Nanjara. Mwinjilisti wa kwanza aliyeachwa kuendeleza kazi ya injili Rombo pamoja na changamoto mbalimbali walizokutana nazo.
Ni Mwinjilisti Eliamlisi Shao kutoka Lole baadae walifuata Wainjisti Aminieli Shao, Amilieli Urio, Mwinjilisti Joseph Silayo Kutoka Nanjara ambaye ni Mwinjilisti wa kwanza mwenyeji pia Mwinjilisti Aminieli Makyao.
Kazi ilipopanuka ulianzishwa mtaa wa Mashati Momwe mwaka 1959 baadae ulianzishwa mtaa wa Rongai mwaka 1963 mtaa huu wa Rongai ulitunzwa na mwinjilisti Danieli Makule kutoka Mamba Kokirie. Mtaa wa Kamwanga ulianzishwa kati ya mwaka 1997 na aliyekabidhiwa kutunza mtaa huo ni Mwinjilisti Penieli Shao Kutoka Lole hadi mwaka 1972 alipokabidhiwa Mwinjilisti Jastini Tarimo kutoka Nanjara ambaye ni Mwinjilisti wa pili mwenyeji.
Mwaka wa 1967 hadi 1974 mitaa hii minne iliongonzwa na kusimamiwa na Mwinjilisti Aminieli Makyao kutoka Mwika Mongai ambaye alipewa leseni maalumu iliyo mwezesha kufanya huduma maalumu za kichungaji kama kubatiza, chakula cha bwana, kupokea wakristo kundini n.k. pia alikuwa kiongozi wa wainjilisti wote Rombo.
Baada ya kazi kuendelea kupanuka Dayosisi iliamua Mitaa iliyopo Rombo iondolewe kuwa misioni ya Usharika wa Mwika na kuwa Misioni ya Dayosisi. Hivyo Mitaa hiyo minne yaani Nanjara, Mashati-Momwe, Rongai, na Kamwanga ikazinduliwa kuwa Usharika wa Rombo mnamo tarehe 04/08/1974 na kukabidhiwa Mchungaji kiongozi wa kwanza Mch: Elias. E. Silayo.
Baada ya usharika huu mpya kuzaliwa mwezi October 1974 ulifanikiwa kununuliwa eneo jipya na kufungua mtaa wa Tarakea mwezi Disemba mwaka 1974 na ukafunguliwa Mtaa mpya wa Mkuu.
Wakristo waliabudia kwenye Jengo lililokuwa la Mahakama ya Wilaya eneo la Ubaa Mwaka 1975 kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya aliyekuepo kwa kipindi hicho walifanikiwa kupata eneo lenye hekari nne lililopo makao makuu ya Wilaya ambapo walifanikiwa kujenga Kanisa, nyumba ya Mchungaji na Hostel.
Ujenzi huo ulipata ufadhili kutoka Ujerumani ambao hayati Askoful Dkt. Stefano Rubeni Moshi aliwapatia Mwaka 1976 kabla hajafariki. Baada ya kufariki kazi hiyo na mahusiano hayo yaliendelezwa na Askofu Dkt. Erasto Kweka hadi ujenzi ulipokamilika mwaka 1983.
Mwaka 1977 ulianzishwa Mtaa wa Useri. Mwaka 1977 mpaka wa Kenya na Tanzania ulifungwa na wakristo wa Kenya waliokuwa wakiabudu Tarakea na Rongai walishindwa kufika kanisani Tanzania, Ikabidi waanzishe Mtaa wao unaoitwa Rongai Kenya eneo la Kariangei ambao sasa ni Usharika wa Loitokitoki Kenya. Mwaka 1978 ulianzishwa mtaa wa Emoritoti na baadaye Orkaswa.
Mwaka 1982 usharika wa Rongai ulianzishwa chini ya Shemasi Joseph Silayo na mwaka 1987 usharika wa Mkuu ulianzishwa chini ya hayati Mch Abide Kanango.
Mnamo mwaka 1993 Usharika wa Imortoti ulianzishwa kutoka usharika wa Rongai na Kiongozi wa kwanza akiwa Mch: Dauson Kaaya.
Kufikia mwaka 2002 Usharika wa Tarakea ulianzishwa kutoka Usharika wa Nanjara Mch: kiongzi akiwa ni Mch: Nelson Machange.
Mpaka sasa Sharika zote za Rombo kuanzia mwaka 1974 hadi leo ni Sharika Tano ambazo zinamitaa 24 ukiondoa Usharika wa Emortoti ambao umehamishiwa Jimbo la Sihaa. Eneo la Rombo ambalo ni Wilaya nzima yenye Tarafa 5, Kata 28, Vijiji 68 na Vitongoji 318 kuna Sharika nne na Mitaa 20 tu.