Mkutano Mkuu wa 17 wa Wanahisa wa Uchumi Commercial Bank (UCB) umefanyika Agosti 12, 2023 Uhuru Lutheran Hotel and Conference Centre.
Akitoa taarifa yake kwa wanahisa wa Uchumi Benki, Meneja wa Benki hiyo CPA. Samwel Wado amesema mtazamo wa benki kwa sasa ni kukuza mtaji kufukia zaidi ya bilioni 15 ambapo ni kiwango cha chini cha Benki ya Dunia kuruhusi kufungua matawi mengine nje ya Mkoa wa Kilimanjaro.
Alisema katika kipindi cha kutekeleza mpango mkakati wa miaka mitano 2018-2022 hususani wa kuongeza ukwasi/mtaji na wateja wamefikia malengo kwa asilimia 66 kutokana na changamoto mbalimbali hasa COVID 19 iliyosababisha kudorora kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi hususani utalii.
Alisema hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2022 benki hiyo ilikuwa na mtaji wa shilingi bilioni 10.2 sawa na asilimia 51 ya mtaji waliokusudia kufikia wa kiasi cha shilingi bilioni 15.
Aidha alisema wataendelea kuimarisha huduma na programu za mawakala kuongeza ufanisi, ubunifu na thamani ya wanahisa.
“Tutaendelea kuboresha huduma na kuendelea kukusanya amana za wateja ili Benki iimarike katika mtaji/ukwasi pamoja na kuongeza jitihada za kuthibiti mikopo chechefu kwa kuongeza kasi katika ukusanyaji wa mikopo” Alisema CPA Wado.
Naye Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kiluther Tanzania na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, ambaye pia ni mwanahisa katika benki hiyo alisema kuwa mwenendo wa Benki ya uchumi UCB unaendelea kuimarika na kukua kwani imeweza kuongeza faida na rasilimali za benki kwa kiasi kikubwa.
Aidha Dkt. Shoo aliwataka wanahisa kuhakikisha wanaendelea kuwekeza kwenye benki ya Uchumi ili kukuza mtaji wa benki na kuiwezesha kufikia malengo na kuwa benki ya kibiashara.
Kwa upande wa mwenyekiti wa Bodi ya UCB Bw.Wilson Ndesanjo alisema benki hiyo itaendelea kuboresha mifumo ya kisasa ya kibenki katika kutoa huduma pamoja na kushiriki huduma mbalimbali za kijamii kama kutatua changamoto mbalimbali katika sekta ya Afya, Elimu n.k.
Bw. Ndesanjo aliwashukuru wote walioshirikiana na Benki kwa mwaka 2022 katika kutekeleza mipango ya benki. Vilevile aliishukuru serikali na Rais kwa kuweka mazingira mazuri ya kibiashara yaliyoiwezesha Benki kufanya shughuli za kibenki kwa Uhuru.
Uchumi Commercial Bank Ltd (UCB) ilianzishwa mwaka 2005 na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzani Dayosisi ya Kaskazini