Mkuu wa KKKT Afungua Semina ya PW Angaza

Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo alifungua semina ya Wasaidizi wa Sharika (Parishworkers) ya Siku 3 iliyofanyika Katika kituo cha Wanawake Angaza Agosti 17-19, 2023.

Akizungumza na Parish workers (PW) hao, Askofu Dkt. Shoo aliwataka kujiamini na kutokuwa na mashaka wanapofanya kazi ya Mungu kwani huduma wanayofanya ni Muhimu katika Kanisa.

Alisema  wasaidizi wa Sharika ni sehemu muhimu sana Katika kanisa la Bwana na Dayosisi inatambua thamani ya huduma yenu.

“Huduma yenu ni muhimu sana kwa uhai wa Sharika, nimeona utofauti mkubwa nilipotembelea Sharika zenye huduma hizi na zisizo kuwa nayo;  pia napenda muelewe Dayosisi naKanisa linatambua sana umuhimu wa huduma yenu na ndiyo maana huduma yenu inatambulika katika katiba ya Dayosisi.” Alisema Dkt. Shoo.

  Aidha Alisema ni vyema wasiwe na hofu kwa kudhani kwamba huduma wanayofanya  haitambuliki  wala kuheshimika na kusema  Kila mmoja anapaswa kujua  huduma yake ni ya muhimu na wala wasikubali mtu yeyote aidharau huduma yenu.

“Kama Neno linavyosema mtambue kuwa huduma hii mmeitiwa na Yesu, na Yesu anatumia njia mbalimbali kutimiza kusudi lake, kwa namna ya kipekee Bwana Yesu alimwita Paulo Katika huduma angali awali alikuwa analitesa kanisa lakini kwa Neema Yesu akamwita akamkabidhi  huduma takatifu”

“Na Paulo kwa kutambua kuwa huduma yake aliitwa kutoka na Yesu, aliifanya pamoja na changamoto mbalimbali alizopitia, nanyi mfanye kama Paulo, fanya huduma yako ukitambua Yesu ndiye aliyekuitia kwa kujiamini”

Kadhalika aliwataka kutoshawishika  kuwatukuza wanadamu wala kuwapendeza wanadamu katika kazi zao bali wafanye kwa bidii na kwa uaminifu kwa utukufu wa Mungu  na Kuzaa matunda mema.

Pia  alisema ni vyema wakawa  kielelezo katika maisha ya ufuasi wa Yesu  na kama kweli ni  wafuasi wa Yesu  wajiulize kama katika kutenda na kuenenda kwao kunaonekana  kama ni wafuasi wa Yesu.

Kwa upande wake Katibu wa Idara ya Wanawake Dayosisi ya Kaskazini Mch. Faustine Kahwa alisema kuwa lengo la kutoa semima imelenga kuwajengea uwezo ili wanapokwenda kwenye sharika zao waweze kutumika kikamilifu.

Na baadhi  ya washiki walioshiriki katika semina hiyo Lilian Robinson kutoka Usharika wa natiro amesema kuwa watajifunza mengi ikiwa ni mambo ya Kiroho na ya kimwili.