Nane wasimikwa kazini

Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro kati Mch. Javason Mrema ameongoza ibada ya kuwasimika kazini wainjilisti 8 wa kanda ya tano jimbo la K/Kati usharika wa TPC Juni 24, 2023. Aliongoza ibada hiyo akishirikiana na Mkuu wa jimbo hilo mstaafu Mch. Kenedy Kisanga, Mch. Asanterabi Munisi, Mch. Emmanuel Chambi na Mch. Kiongozi wa Usharika huo Mch. David Pallanjo.

Akihubiri katika ibada hiyo Mkuu wa jimbo mstaafu Mch. Kisanga alisema anafurahi kuwaona wainjilisti wapya wanaokwenda kusimikwa na kwenda kutumika katika shamba la Bwana.

Alisema kanisa linakuwa kwa sababu ya kazi kubwa inayofanywa na wainjilisti. Wainjilisti wamefanya kazi kubwa ya kuhubiri na kulikuza kanisa na ndiyo maana sharika zina kuwa na kuzaa sharika nyingine alieleza Mch. Kisanga

Alisema  watumishi hawa wamepewa utume wa Yesu ulio hai kupeleka ujumbe wa neno la Mungu. a Utume huu hauji kwa bahati bali ni roho mtakatifu ndiye anayefanya kazi ya kuchoche wito na hatimaye mtu anaamua kukata shauri na kumtumikia Mungu.

“Ninyi wainjilisti Mungu amewaita kutumika katika kanisa la Mungu, msidhani mmeitwa kutumika katika usharika wa magadini tuu, ni popote ulimwenguni kuhubiri injili”Alisema Mch. Kisanga.

Aliwaamba wanapaswa kuwahubiria watu neno la Mungu, watubu na kupokea tabia mpya ya kuwa na maadili mema na kuwa wacha Mungu wapate kuingia katika Ufalme wa Mungu.

“Yesu anawatuma mitume ili kuendeleza na kukamilisha kazi yake ya kuwafanya watu wote kuwa wana wa Mungu nanyi mnaosimikwa leo mtambue wajibu wenu na kama wa hawa mitume.

Mmepewa kazi ya kuingia katika kanisa la Mungu na kuubadilisha ulimwengu wote kuwa wanafunzi na wafuasi wa Mungu kwa kulifundisha neno la Mungu” Alisema Mch Kisanga.

“Tunayo kazi kubwa ya kulihubiri neno la Mungu na tunapaswa kujiuliza kama kweli tunapeleka ujumbe wa neno la Mungu kwa usahihi au tunachakachua kuwafurahisha watu”

Alisema ujumbe tunaopaswa kuupeleka kwa watu ni kuwa sisi sote ni wenye dhambi na tunapaswa kuwaambia watu watubu wakapate kupona. Wainjilisti mnapaswa kupeleka injili bila woga,  msimame kwa ushujaa, vaeni mavazi yenu mkatoe neno la Mungu kwa umahiri alieleza.

“Simama kama ulivyo, usiige mna neno la Mungu, mnaliturugia ya kilutheri, ifuateni, muache kuiga taratibu za ibada zisizoeleweka”. Alisema Mch. Kisanga.

Alisema tunapokwenda kuwatumikia watu, msiende kuwa wasemaji tu bali mkawasikilize watu maana wana majeraha na shida zao.

“Wainjilisti muwe na masikio ya kuwasikiliza watu, watu wanamajeraha na mkifanya hivyo watu watakuja kanisani, watu wana mambo mengi yanayowasumbua na wanahitaji kusikilizwa na kutatuliwa matatizo yao”

Mara baada ya mahubiri Mkuu wa Jimbo aliwasimika rasmi wainjilisti hao na kuwakumbusha kuwa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzani linaongozwa na neno la Mungu na katiba.

Kawataka washarika kuwapa heshima na ushirikiano wainjilisti walioingizwa kazini ili kazi ya Bwana isonge mbele.

Akitoa salam za jimbo mkuu wa Jimbo Mch. Mrema alimshukuru Mungu kwa baraka ya watumishi waliongizwa kazini. Kawasihi wainjilisti kulishika neno la Mungu maana neno la Mungu ndilo taa na njia. Ukumbuke Mungu ndiye aliyekuita na sii mwanadamu hivyo mkatumike kwa bidii na uaminifu.

Kawaomba wainjilisti na watumishi wote kutimiza wajibu wao bila kutega “ Usifanye pale unapomwona kiongizi wako tuu. Pia kawaomba wahubiri kweli ya neno la Mungu, wajiandae vizuri kufundisha neno maana wamefundishwa darasani” Alisema Mch Javason.

“Tumia kipawa chako ulichopewa na elimu uliyonayo kuhubiri kweli ya neno la Mungu na kuimarisha mitaa yenu kwa kuwaimarusha washarika. Muwe na maono na malengo mazuri katika mitaa na sharika zenu”.Alihimiza

Pia wataka wainjilisti na viongozi wa Kanisa kuwa mfano wa kuigwa katika suala la uwakili wa muda, kutoa n.k. Anasema washarika wakiona kiongozi anajitoa na wao watajitoa kwa moyo.

Mch. Kiongozi wa Usharika wa TPC Mch. David Pallanjo aliwashukuru washarika na kuwatakia baraka za Mungu wainjilisti wapya katika kutumika kwao