Zaidi ya Walimu Wakuu 70 na Maafisa Elimu 6 wa Shule za Montessori Wakutana Ushirika wa Neema.

Zaidi ya walimu wakuu 70 na maafisa elimu 6 wa shule za msingi wilaya ya Siha Mkoani Kilimanjaro wamekutakana kwenye warsha ya siku moja katika chuo cha waalimu  wa Montessori cha Ushirika wa Neema kwa  lengo la kujengeana uwezo wa ufundishaji hususani kwa matumizi ya vifaa mbalimbali vya ufundishaji kwa njia ya vitendo katika shule za awali za Serikali.

Mkuu wa chuo cha Montessori cha Ushirika wa Neema wa Masista wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini, Sr Christina Nakei alisema wamelenga kujengeana uwezo na kushirikishana mambo mbalimbali katika kuwajenga watoto na kuwafunza katika ngazi za awali, chekechea na msingi.

Pia amesema warsha hiyo imelenga kuwaonyesha waalimu mafunzo wanayotoa chuoni hapo kwa ngazi ya chati kwaajili ya kuwafundisha watoto wadogo kwa njia ya vitendo kwa kutumia dhana/vifaa vya kufundishia kwa njia ya vitendo kwa madarasa ya Montessori ili wale walimu wa shule za serikali waweze kupata mbinu za kuwafundisha watoto.

 “Lengo kuu la warsha hii ni walimu kuweza kuona madarasa ya vitendo na dhana za kufundishia na ninatumaini kuwa babada ya waalimu wakuu kupata mafunzo haya watawaleta waalimu kupitia mwongo uliotolewa na wa serikali wa kuongeza elimu kwa watumishi makazini ili kupata taaluma hii ya mafunzo yatakayoboresha ufundishaji wa watoto”Alisema Sr Christina.

Sr Christina alisema mfumo wa kufundisha kwa njia ya vitendo ujulikanao kama montessori unamwezesha mtoto kujifunza vitendo mbalimbali kwa kuona au kushika ambapo mzazi au mlezi anaweza asitambue kwa urahisi. Anasema elimu kwa njia ya vitendo inampa uwezo mkubwa katika utendaji na unamsaidia kuwa huru katika utendaji, ufumbuzi na kuwa makini katika maisha.  

Naye Mwalimu Mkuu Dickson Mlay kutoka shule ya Msingi Lawate anasema wanashukuru kwa mwaliko waliopata kutoka chuo cha Montessori Ushirika wa Neema kwa ajili ya kujifunza namna ambayo wanafunzi wanaandaliwa kujifunza kwa njia ya vitendo na kwa kujitegemea pasipo kumtegemea mwalimu kwa kiasi kikubwa.

Naye Mkufunzi wa chuo cha Montesori Ushirika wa Neema ambaye pia ndiye Mratibu wa mafunzo ya montesori Dayosisi ya Kaskazini Bibi. Shose Ngowi amesema mbinu ya kufundishia inayosisitiza kujitegemea na uhuru wa kujifunza lakini wenye mipaka. Mbinu hii ni ya kisayansi kabisa na inazingatia saikolojia  katika maendeleo  ya kukua kwa mtoto kimwili, kiakili, kimhemko (Kihisia), kijamii na kiroho.

Ni mbinu inayozingatia maendeleo ya maarifa kwa kuzingatia mazingira ya asili. Mbinu hii mwalimu huwa mwelekezaji tuu ili kumwezesha mtoto kufikia uwezo wake wa juu kabisa katika ujifunzaji au kupata maarifa

Falsafa hii ya malezi, makuzi na ufundishaji kwa njia ya mtoto kufanya mwenyewe ilianzishwa na Dkt. Maria Montessori huko Italia ambaye alikuwa ni Daktari wa afya ya akili  Dkt. Maria alizaliwa mwaka 1870 na alifariki 1952 huko Italia. Aliweza kutumia mfumo huu wa kujifunzia na kupata maarifa kupitia  milango mitano ya maarifa kwa kutumia zana kwa watoto wenye utindio wa akili na kuleta matokeo chanya. Ndipo alipoona kwamba ikiwa kwa mtoto mwenye utindio matokeo ni mazuri hivi itakuwaje kwa yule ambaye hana tatizo.

Warsha hiyo ilifunguliwa kwa sala iliyofanywa na  Mch. Rickenson Moshi Katibu wa Elimu ya Kikristo KKKT Dayosisi  ya Kaskazini.

Alisema ni jambo lililojema kurisishana taaluma na ujunzi “Unapokuwa kiongozi ni vyema kuhakikisha kuwa katika nafasi uliyonayo ni jambo lililojema kumwandaa mtu atakayeshika nafasi yako wakati ambao hautakuwepo”. Alisema Mch. Moshi.