BCC: TANO  wenye Ulemavu wa Akili wahitimu mafunzo ya ujuzi

Ni siku ya kipekee kwa vijana 5 wenye ulemavu wa akili wanaohudumiwa na kitengo cha Building A Caring Community (BCC) cha KKKT Dayosisi ya Kaskazini kuhitimisha mafunzo yao kupitia mpango wa Vijana wa mafunzo ya ujuzi wa shughuli mbalimbali za mikono.

Kwa mujibu wa mratibu wa mafunzo hayo Bibi. Jeska Kileo, ameeleza kuwa program hiyo hutolewa kwa vjana wanaoandaliwa kujitegemea wenye umri wa kati ya miaka 12-22. Amesema mafunzo hayo hutolewa kwa miaka 3 hadi 4 kulingana na uwezo wa kijana kuelewa kile anachofundishwa.

Alitaja  ujuzi wanaopatiwa ni pamoja na shughuli za Kilimo Cha mboga, ufugaji wa kuku, utengenezaji wa sabuni, kadi, shanga, zulia pamoja na vigae.

Naye mratibu wa kitengo cha BCC Dayosisi ya Kaskazini, Mdiakonia Elirehema Kaaya akizungumza katika  mahafali hayo alisema, vijana hao wamemaliza ‘program’ zote zinazotolewa na BCC zikiwemo tiba tengamao, elimu ya kujitambua, kujenga fikra chanya kuhusu maisha yao na ya mwisho  programu ya vijana ya mafunzo wa ujuzi katika fani mbalimbali.

Aliwahimiza wahitimu hao kuwa, wanaporudi katika familia zao, wakatumie vizuri ujuzi walioupata   kwa kufanya kazi kwa bidii kwa manufaa yao, familia na jamii. Pia aliwataka wazazi na walezi wa vijana hao kuendelea kushirikiana na BCC, kuhakikisha Vijana hao wanaendeleza ujuzi na miradi waliyoianzisha

Huduma ya kuwahudumia watoto na vijana wenye ulemavu wa Akili inatolewa na KKKT Dayosisi ya Kaskazini kupitia Idara ya Udiakonia kitengo cha Bulding A Caring Community wakishirikiana na shirika la MOSAIC la Nebraska  

Wahitimu 5 wenye vyeti walipohitimu mafunzo ya ujuzi wa shughuli mbalimbali za mikono yanayotolewa kwa vijana wenye umri kati ya miaka 12-22 wenye ulemavu wa akili.