Mkutano Mkuu wa 43 Elimu ya Afya ya Msingi Wafanyika

Msaidizi wa Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini, Mch. Deogratius Msanya amefungua Mkutano Mkuu wa 43 wa Elimu ya Afya ya Msingi katika ukumbi wa Mikutano wa Umoja Lutheran Hostel April 6, 2024.

Neno la ufunguzi lilitoka katika kitabu cha  Zaburi ya  107:19-20..  “Wakamlilia BWANA katika dhiki zao, Akawaponya na shida zao. Hulituma neno lake, huwaponya, Huwatoa katika maangamizo yao.”


Akizungumza katika ufunguzi huo, Mch Msanya ambaye ndiye mwenyekiti wa mkutano aliwakumbusha wajumbe kuwa, Elimu ya Afya ya Msingi imedhamiria kumhudumia mwanadamu katika ukamilifu wake yaani kimwili, kiakili, kiuchumi na kiroho.

Alisema ni vyema kuzingatia katika kipindi hiki ambacho jamii inakabiliwa na changamoto nyingi katika maisha hasa uhaba wa ajira kwa vijana, wanawajibu mkubwa wa kuisaidia jamii kukabiliana na changamoto hizo.

Alisema uhaba wa ajira kwa vijana kumepelekea vijana wengi kujiingiza katika ulevi wa kupindukia… Kijana anaamka anatafuta pombe badala ya kufanya kazi, anaanza kunywa tangu asubuhi hii ni hatari kubwa kwa afya ya mwili na ya Roho, tuwasaide.”


Kama neno linasvyosema watu wa Mungu walimlilia Mungu katika dhiki zao naye akawaponya, nasi tuwakumbushe watu kumlilia Mungu na kuwaelekeza namna ya kutatua changamoto zao za kiuchumi, kiafya na kiroho pia.


Mch. Msanya alisema kwa sasa magonjwa yasiyoambukiza yamekuwa ya hatari kubwa sana, magonjwa haya ni silence killer, watu wanaishi na magonjwa kama presha, sukari na siku anapima anasema sikuwaga na presha lakini kumbe amekuwa na shida hiyo kwa muda mrefu.


Aliwataka waratibu katika majimbo kuweka jitihada katika kununua vifaa vya kupima magonjwa kama presha, sukari n.k ili wanapotoa Elimu na watu kuhamasika kupima afya zao waweze kufanya hivyo.


Kwa mujibu wa Katibu wa Afya wa Dayosisi ya Kaskazini Bw. Joshua Ndaga alisema katika mkutano huo kuna wajumbe takribani 75 ambao ni waratibu wa Elimu ya Afya ya Msingi  kutoka majimbo tano ya Dayosisi ambayo ni pamoja na Jimbo la Kilimanjaro Kati, Kilimanjaro Mashariki, Siha, Hai na Jimbo la  Karatu.


Alisema miongoni mwa mambo watakayoyajadili ni kuhusu uhamasishaji wa kamati za afya sharikani, utoaji wa taarifa za kazi sharikani, changamoto zinazowakabili pamoja na kuongezeka kwa magonjwa yasiyoambukiza.


Mambo mengine ni pamoja na kujadili matumizi ya taarifa kulingana na huduma wanazotoa, mahusiano katika ngazi ya Sharika, Jimbo, Dayosisi, wahisani, na wadau mbalimbali wa Afya.


Kwa upande wake Mratibu wa Elimu ya Afya ya Msingi Bi. Isaria Megiroo alisema pamoja na mafanikio waliyopata  kumekuwepo na changamoto ya uhaba wa vitendea kazi kwa upimaji wa shinikizo la damu, uzito na sukari. Pia suala la usafiri kwa waratibu limekuwa na changamoto ambapo mwenyekiti amehimiza kuzingatia ratiba na ratiba iheshimiwe kuepuka mwingiliano.