Katibu Mkuu wa LWF afanya ziara kuona Maendeleo ya Kanisa Afrika, Kaanzia Tanzania.

Katibu Mkuu wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri  Duniani Mch. Anne Burghardt ametembelea Bara la Afrika na kuanza na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzani (KKKT) kuona maendeleo ya Kanisa ikiwa ni ziara yake ya kwanza tangu achaguliwe kushika wadhifa huo Mwezi Juni, 2021

Kufuatia ziara hiyo, Machi 26, 2022 Mch. Anne alitembelea Makao Makuu ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini na taasisi mbalimbali za Kanisa na Dayosisi ambapo Jumapili Machi 27, ameshiriki Ibada ya Jumapili katika Kanisa Kuu la Moshi Mjini.

Taasisi alizozitembelea akiongozwa na mwenyeji wake Askofu Dkt. Fredrick Shoo ni pamoja na Hospitali ya KCMC  ambapo aliweka jiwe la msingi la hosteli ya wagonjwa wa Kansa.

Taasisi nyingine ni benki ya Uchumi Commercial Bank (UCB), Kituo cha Masista wa Ushirika wa Neema na redio Sauti ya Injili.

Mch. Anne Burghardt

Ni mwanamke wa kwanza kushika wadhifa wa Katibu Mkuu wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani na mtu wa kwanza kutoka bara la Ulaya ya Kati-Mashariki tangu kuanzishwa kwake mwaka 1947.

Yeye ni msharika wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Estonia. Alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu katika Baraza Kuu la Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani tarehe 19 Juni 2021 na kuanza rasmi wajibu huo tarehe 1Novemba 2021. Fungamano la Makanisa ya Kiinjili ya Kilutheri Duniani lina Makanisa wanachama 148 katika nchi 99 duniani na waumini wanaokadiriwa kuzidi milioni 77 kwa takwimu za mwaka 2020.

Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania ni Kanisa la 3 kwa ukubwa likitanguliwa na Kanisa la Mekane la Ethiopia na kufuatiwa na Kanisa la Sweden. Mch. Anne ana asili ya nchi ya Estonia. Wakati wa kupokea kijiti kutoka kwa mtangulizi wake Mch. Dkt. Martin Junge. Mch. Anne alisema: “Ninasali kwamba kazi yangu itakuwa na mchango katika kukua pamoja kwa Makanisa haya [wanachama] tunapokusanyika kwa Yesu Kristo, ambaye anatuunganisha wote katika dhamira yetu kwa dunia” (nukuu hii si ya moja kwa moja).

Aidha, Mch. Anne anasimamia utekelezaji wa mkakati wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani (2018-23) uitwao kwa Kiingereza“With Passion for the Church and for the World” tafsiri isiyo ya moja kwamojani “Kwa Shauku kwa ajili ya Kanisa na kwa ajili ya Dunia” unaoweka mkazo katika Kanisa kujihusisha na masuala ya mabadiliko ya tabia nchi, mitandao ya kithiolojia na fursa mpya za ushirikiano, udiakonia, ekumene, usawa wa jinsia na masuala ya vijana.

Fungamano hili linaongozwa na rais ambaye kwasasa ni Ask. Musa Panti Filibus kutoka Kanisa la Kilutheri la Nigeria.

Katibu Mkuu wa LWF Mch. Anne Burghardt akisaini kitabu cha wageni alipowasili ofisi kuu ya Dayosisi Machi 26, 2022