Kilele Juma la Afya Chafanyika Fuka

Kilele cha Juma la Afya Kidayosisi kimefanyika na kufungwa rasmi na Mhe. Msaidizi wa Askofu, Mch. Deogratius Msanya Julai 25, 2022 katika Usharika wa Fuka Jimbo la Siha la KKKT Dayosisi ya Kaskazini.  Katika Ibada hiyo liliandaliwa somo kuhusu ugonjwa wa Homa ya Ini, njia ya maambukizi na Chanjo ya kujikinga.

Akifundisha kuhusu homa ya Ini na chanjo yake, Dkt. Joseph Temba kutoka Hospitali ya wilaya ya Siha alisema Homa ya Ini ni ugonjwa ambao unaambukizwa kwa njia mbalimbali ambazo mojawapo alitaja kuwa ni kwa kuwekewa damu ya mtu mwenye virusi vya Homa ya Ini, kuchangia vitu vya kutobolea masikio au pua, sindano, nyembe nk. Njia nyingine alitaja kuwa ni kwa kujamiana na mtu mwenye maambukizi.

Dkt. Temba alisema ugonjwa huu hauna tiba hivyo ni muhimu kupata chanjo ya kujikinga dhidi ya maambukizi. “Chanjo ni muhimu kwa ajili ya kuzuia magonjwa katika miili yetu hata Mungu alipomuumba mwanadamu alimpa kinga ya mwili na kumpa mwanadamu maarifa ya kutengeneza kinga ambayo tunaipata kwa njia ya chanjo”.Alisema Dkt. Temba

Aidha alisema chanjo hiyo inafaa kwa mtu aliyepima na kubainika hana maambukizi. Anasema kwa mujibu wa maelekezo ya wizara ya Afya chanjo ya Homa ya Ini inatolewa kwa gharama ya shilingi 20,000/= kwa ajili ya kupima na chanjo.

Katika kilele hicho Kamati ya Afya Jimbo la Siha waliandaa banda la maonyesho lenye vyakula vya asili kama somo na msisitizo wa watu kutumia vyakula vya asili kwa afya bora.

Neno la mahubiri lilitolewa na Mhe. Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya ambapo alikaza kuhusu Upendo kwa wanadamu. Alisema tunapaswa kuutafsiri upendo kwa njia ya matendo yetu sisi kwa sisi.

“Upendo ni vitendo, ni matendo ya ukarimu kwa wenzetu na upendo unapokosekana mahali hapafai kukaa, watu wakikosa upendo wanaweza kuangamizana kwa sababa ya kukosa tabia ya Mungu ya Upendo.”Alisema Mch. Msanya.

Akihitimisha mahubiri yake Mhe. Msaidizi wa Askofu alimshukuru Dkt. Temba kwa somo alilofundisha na kuhimiza umuhimu wa kuwa mawakili wazuri wa Afya zetu akinukuu usemi usemao Kinga ni bora kuzidi tiba.

Mhe. Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya(wa kwanza kushoto mwenye kola ya kichungaji) na Mhe. Mkuu wa Jimbo la Siha Mch. Elisa Kileo (wa kwanza kulia na mwenye kola ya kichungaji) kwenye banda la maonyesho la Kamati ya Afya Jimbo la Siha walipolitembelea mara baada ya Ibada