Mahafali ya 70 Yafanyika Mwika, 70 Wahitimu,

Mahafali ya 70 Yafanyika Mwika, 70 Wahitimu,

Mch. Overa Suhlberg Astaafu kwa Heshima,

Atumika miaka 31.

Askofu Dkt. Shoo Awataka wahitimu Kutumika kwa Uaminifu

Mkuu wa KKKT na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo ametoa vyeti kwa wahitimu 70 katika mahafali ya 70 ya Chuo cha Biblia na Theologia Mwika Oktoba 20, 2023.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Chuo cha Biblia na Theologia Mwika Mch. Obed Akyoo alisema, wahitimu waliothibitishwa kuhitimu katika kozi mbalimbali ni pamoja na wahitimu 37 wa kozi ya Elimu ya Kikristo na Uinjilisti ngazi ya cheti, 14 wamehitimu kozi ya Wasaidizi wa Sharika Huduma za Jamii ngazi ya cheti, 10 kozi ya muziki wa Kanisa ngazi ya cheti. Wengine ni 3 Kozi ya Muziki ngazi ya Stashahada na 6 walihitimu kozi ya Theologia ngazi ya Cheti.

Kabla ya kuwatunuku vyeti wahitimu hao Askofu Dkt. Shoo aliwataka wahitimu hao kwenda kwenye utumishi na huduma waliyoitiwa na  Mungu na kutumika kwa uaminifu wakitambua nguvu yao itatoka kwa Yesu pekee.

Alisema wawapende wale watakaowahudumia na kuwahudumia kwa bidii na kwa uaminifu bila ubaguzi kama wafuasi wa Yesu Kristo. “Msiende kufanya mambo ya usanii kama wanaofanya baadhi ya watumishi” Aliwataadharisha Askofu Dkt. Shoo

Mchungaji Overa Suhlberg Astaafishwa kwa Heshima.

Katika ibada hiyo ya mahafali ya 70, Mkuu wa Kanisa na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Shoo alimstaafisha kwa heshima Mchungaji Overa Suhlberg baada ya kutumika katika huduma ya kichungaji kwa miaka 31.

Mchungaji Overa alianza huduma ya kichungaji mwaka 1992 ambapo alitumika katika kanisa la Kulutheri nchini Sweden mwaka 1992-2013. Baada ya kutumika Nchini Sweden mwaka 2014 hadi anastaafu alikuwa Mkufunzi wa Chuo cha Biblia na Theologia Mwika.