Mkutano Mkuu wa 16 wafanyika Hai

  • Mkutano Mkuu wa 16 wafanyika Hai
  • Jiwe la pembe lawekwa kituo cha malezi
  • Askofu Shoo Ahimiza Umoja

Mkutano Mkuu wa 16 wa Jimbo la Hai umefanyika Oktoba 11, 2023 katika bustani ya Jimbo ambapo ulifunguliwa rasmi na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania na Dayosisi ya Kaskazini, Askofu Dkt. Fredrick Oanel Shoo. Katika mkutano huo taarifa ya jimbo ilitolewa  na Mkuu wa Jimbo na kujadiliwa na wajumbe toka sharika zote za Jimbo kisha kuweka maazimio na mipango mbalimbali ya Jimbo.

Mkutano huo uliambatana na  uwekaji wa jiwe la pembe kituo cha kutwa cha malezi ya watoto (Day care) tendo lililoongozwa na Mkuu wa Kanisa ambapo Katibu wa Jimbo Mwinjilisti Erinest Massawe alisema kuwa, wazo la ujenzi wa kituo hicho ni kuonekana kuwepo kwa uhitaji wa vituo hivyo kutokana na idadi ya watu na watoto kuongezeka.

Akifundisha neno kuu la mkutano Askofu Dkt. Shoo  alisema kuwa umoja na ushirikiano ni jambo la msingi na lakuzingatia katika kujenga mwili wa Kristo  yaani Kanisa.

Askofu Shoo amesema hayo wakati alipokuwa akifungua mkutano Mkuu wa 16 wa Jimbo hai Dayosisi  ya Kaskazini iliyofanyika jimboni hapo mkoani Kilimanjaro.

Alisema  ndani ya mwili wa Kristo Kuna vipawa na karama nyingi ambavyo vikitumika kwa umoja bila ubinafsi kuna kuwa na ufanisi katika utendaji kazi kwenye Sharikani, Jimbo  na  Kanisa kwa ujumla.

Sambamba na hayo alisema kuwa semu ambayo ilitakiwa kujengwa mwili wa Kristo imegeuka na kuwa  sehemu ya mafarakano kutokana na kutokutambua kwamba karama zote zinatoka kwa Mungu na tunazipata kwa Neema tu.

Kwa upande wake Katibu wa Dayosisi ya Kaskazini Mhandisi Z.S Moshi amewataka viongozi mbalimbali wa Jimbo kunia pamoja na kufanya kazi kwa pamoja na kuweka ubinafsi pembeni.

Naye Mkuu wa Jimbo la Hai mchungaji Biniel Mallyo alisema kuwa Jimbo la Hai limefanikiwa katika nyanja mbalimbali ambapo amewataka watumishi wa Jimbo kudumisha utulivu waweze kufanya kazi ya Mungu kwa furaha.