Mkutano wa Wachungaji wafanyika Uhuru Hotel, Mada Uchungaji na Uongozi yafundishwa

Mkutano wa Wachungaji wote walipo kazini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kasakazini, umefanyika Disemba Mosi, 2022 Uhuru Lutheran Hotel & Conference Center.

Mkutano huo uliongozwa na Mwenyekiti Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo mbali na mada za kichungaji pia walijifunza mada inayohusu Uchungaji, Uongozi na Utawala.

Katika mada  hiyo iliyowasilishwa na Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Mhandisi Zebhadia Moshi, alisema masuala ya uongozi na uwajibikaji yanaonyeshwa katika Biblia.

Anasema Biblia ni kama mwongozo wa maisha ya kiroho na yasio ya kiroho akitoa mfano kutoka kitabu cha Hesabu 27:15-20 pale Musa alipomwomba Mungu amchagulie kiongozi wa kumrithi na katika uwajibikaji akatoa mfano wa watumishi waliopewa talanta mmoja akaichimbia chini.

Mhandisi Moshi anasema mchungaji katika usharika ndiye kiongozi na mtendaji mkuu maana ana watu anao wasimamia, ana raslimali watu na anapaswa kuukuza usharika wake. Mchungaji anabeba dhamana ya kuongoza usharika akishirikiana na wenzake.

Anasema mambo wanayokutana nayo wachungaji  ni mapana na yanahitaji ujuzi. “Majukumu ya wachungaji ni mengi sana na ni lazima mchungaji awe na ujuzi na vipawa vingi ‘Multi-Skill’

Vile vile alisema kiongozi mzuri anapaswa kutumia ushawishi zaidi kuliko amri. “Watu wakishawishiwa vizuri kazi nyingi zinafanyika, mjenge matumizi ya ushawishi”. Alisema Mhandisi Moshi.

Pia anasema katika utawala bora ni muhimu kuwa na mpango kazi utakaokuwezesha kujua nini unachopaswa kufanya na kwa wakati gani.

Mkutano wa Wachungaji Disemba 1, 2022 Uhuru Lutheran Hotel & Conference Center