Siku ya Maombi ya Dunia yafanyika.

Siku ya Maombi ya Dunia imefanyika katika Ibada ya asubuhi kwenye chepo ya Ofisi Kuu KKKT Dayosisi ya Kaskazini Machi 3, 2023. Ibada hiyo iliongozwa na Mch. Faustine Kahwa Katibu wa Idara ya Malezi Dayosisi, Mch.Rickenson Moshi Katibu idara ya Elimu ya Kikristo, Mwjst. Elizabeth Mwanjala wakishirkiana na baadhi ya watumishi wa Ofisi kuu.

Akihubiri katika Ibada hiyo, Katibu wa Idara ya malezi Mch Faustine Kahwa ameitaka jamii kurudi na kusimamia mifumo ya asili kama lilivyokuwa kusudi la Mungu alipoumba ulimwengu.

Alisema tunapaswa kusimama na kumwomba Mungu atuwezeshe kurudi na kusimama katika kusudi lake, pale alipotuumba. “Tukiamini na kutambua upana, kimo na ukuu wa Mungu, anaweza kuleta mabadiliko na kurudi kama ilivyokuwa awali”

Kawataka wanawake kumlilia Mungu kwa dhati ili aturejeshe katika maadili mazuri hususani tabia inayokuwa kwa kasi ya ushoga na usagaji.

Miongoni mwa mambo yaliyoombewa ni pamoja  na kuombea familia, malezi, hali ya hewa, Mungu atuepushe kutoka majanga, kumcha Mungu kwa wanataaluma na Wanasayansi. Maombi mengine ni pamoja na amani na utulivu na mafanikio kwa mtu mmoja mmoja, familia, kanisa, taifa na ulimwengu kwa ujumla.

Mwongozo wa Siku ya Maombi ya Dunia mwaka huu umeandaliwa na kamati ya siku ya maombi ya dunia ya Taiwan na kutafsiriwa na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) Idara ya Wanawake Watoto na Jinsia. Neno kuu Waefeso 1:15-19.

Wakwanza Kushoto ni Katibu Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mhandisi Zebadiah Moshi na watumishi wa Ofisi Kuu kwenye Ibada ya Maombi ya Dunia kwenye Chepo ya Ofisi Kuu, Machi 3,2023