Umoja wa Wanaume wazinduliwa Hai, Wapata zaidi ya milioni 21 kutunisha mfuko wao

Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, Mkuu wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini alizindua Umoja wa Wanaume Jimbo la Hai la Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania Dayosisi ya Kaskazini.
Ibada hiyo ilifanyika Machi 24 katika Usharika wa Hai Mjini ambapo pia waliingizwa kazini viongozi wa Umoja huo pamoja na harambee ya kutunisha mfuko wao ambapo kiasi cha shilingi zaidi ya milioni 21 zilipatikana.
Awali Askofu Dkt. Shoo aliwapongeza wanaume wa Jimbo hilo kwa kuwa na maono na utayari wa kuanzisha Umoja wa wanaume.
Alisema imezoeleka  miaka mingi kusikia Umoja wa kina mama katika sharika, jimbo na hata Umoja wa wanawake kitaifa lakini Umoja wa Wanaume umekuwa nadra kusikika.
“Hii ni labda tulifikiri sisi hatuna haja ya Umoja na Umoja ni kwa wanawake ambao baadhi ya mila potofu  ziliwafanya kuteswa na kunyanyaswa na wanaume…wakaona ni bora  waanzishe Umoja wao waweze kufarijiana na kusaidiana.
…Lakini sasa Mambo yamebadilika, wapo wanaume wanaoteswa, wanapigwa na kunyanyaswa na wake zao.”

Alisema wanaume tujiulize tuko wapi, tunafanya nini, nafasi yetu ipo wapi, kama tumesahau tujikumbushe na kushika nafasi zetu katika Familia, Kanisa na Jamii.
…Hatusemi turudi katika mila potofu za kuwakandamiza wanawake laa!!, ni kurudi na kusimama katika nafasi zetu.
Mungu ametuumba mwanaume na mwanamke lakini tumefikia mahali tume changanyikiwa. Vijana wetu wamefikia mahali hawajitambui tena kama ni wanaume, wanajiingiza katia mambo ya ajabu.”
Alisema wanaume kupitia Umoja wao wakishirikiana na wanawake wataweza kufanya familia zao kuwa imara. Tusitarajie kuwa na familia,  jamii au Kanisa lenye afya kama wanaume hatutasimama katika nafasi zetu.
Aidha Dkt. Shoo alisema kuanzishwa kwa Umoja wa wanaume kumekuja kama itikio la wanawake na hili limefanywa na Idara ya wanawake ya Dayosisi ya Kaskazini.
Alihimiza kuwa Umoja huo unawahitaji wanaume imara, jasiri ambao wataweze kukumbushana juu ya wajibu wao hasa wa kukaa na watoto wakiume kuwafundisha  na kuwaanda kuja kupokea majukuma ya familia.
“Tunapaswa kuwaandaa watoto wakiume ili waweze kushika nafasi zao watakapofikia umri wa kushika majukumu ya mwanaume kama baba.
…Vijana wamekuwa legelege, kijana ameo bado anakaa kwa baba anakula kwa baba, wanaume mashujaa tunapaswa kusimama kama mashujaa wenye maadili ili watoto wetu waige”Alisema Dkt. Shoo
Kadhalika alisema kupitia Umoja huo wanaume wakumbushane kuwa na hofu ya Mungu, tukiwa wenye hofu ya Mungu tutatimiza wajibu wetu vizuri kama viongozi wa mambo ya Imani katika familia zetu.”