Utandawazi usikupotezee muda: Mdiakonia Bariki Mlaki

Mdiakonia Bariki Mlaki ambaye ni Kaimu Katibu wa Idara ya Udiakonia ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini amewatahadhrisha vijna kutokupoteza muda wao kutumia utandawazi katika mambo yasiyofaa na badala yake wautumie utandawazi katika mambo chanya.

Akiwasilisha mada inayohusu faida za utandawazi kwenye Juma la Askofu na Vijana Disemba 13, 2022, alisema utandawazi ukitumika vizuri unafaida kubwa katika kurahisisha mfumo wa maisha katika ulimwengu wa sasa.

Alisema utandawazi umekuwa na faida nyingi kubwa akizitaja kuwa ni pamoja na kuifanya dunia kuwa karibu/kijiji kimoja, kuwasaidia watu wa kada mbali mbali kujiendeleza kimasomo, kibiashara na hata kufahamiana.

Pia alizitaja faida nyingine kuwa ni pamoja na kuimarisha suala la ulinzi na usalama akitoa mfano wa kamera za ulinzi (CCTV Camera), uharaka wa kupashana habari na urahisishaji wa masuala ya kibiashara.

Alisema faida nyingine ni kuwezesha watu kubadilishana ujuzi na maarifa na hata kutanua wigo wa uwazi na kufichua vitendo viovu kwa urahisi na haraka.

Mlaki alisema pamoja na faida zilizopo, utandawazi kwa upande mwingine umeleta hasara kubwa katika suala la kimaadili katika jamii hususani kwa watoto na vijana ambao wazazi na walezi wao wanapokosa muda wa kuwa nao kuwaelimisha na kuwaelekeza matumizi sahihi yenye maadili na manufaa kwa jamii.

Anasema utandawazi hasa katika mitandao ya kijamii umeondoa utu wa mtu/watu, tamaduni, kuharibu faragha (Privacy) ya mtu na kulazimisha watu wote kuwa na mitazamo na akili zinazofanana.

Mlaki anasema licha ya kuwa na faida katika kueneza habari lakini wapo baadhi ya watu wanatumia fursa hiyo kueneza habaari za uwongo na uzushi unaosababisha mitafaruko katika jamii na wakati mwingine kusababisha magomvi, vifo na maumivu katika jamii.

Aidha aliwaasa vijana kutumia utandawazi vizuri lasivyo wataishia kupoteza muda, fedha nyingi, mwelekeo wao katika maisha na kuwa na kizazi cha ovyo kisicho na maadili wala mwelekweo chanya wa maisha.

“Niwaombe vijana hasa wale mnaotumia simu janja (Smart phone) au vishikwambi n.k, mvitumie katika kujifunza na sio kuiga mambo yasiyo na maadili. Vijana wengi wanaangalia picha za ngono, wanajifunza mambo machafu ambayo yamewagharimu vijana wengi; wamejiingiza katika mapenzi ya jinsia moja, n.k jambo linalowasumbua watu wengi ambao walijaribu na hata sasa wengine wapo kwenye ndoa lakini bado wameshindwa kuacha hizo tabia. Ninawaambia msithubutu ” Alisema Mdiakonia Mlaki.