Mkuu wa KKKT na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo aliongoza kikao cha Wanadayosisi waliopo Safarini (Diaspora) Disemba 27, 2023 Uhuru Lutheran Hotel& Conference Centre kikao ambacho hufanyika kila mwisho wa mwaka kujadili masuala mbalimbali yahusuyo maendeleo ya Dayosisi.

Sambamba na kikao hicho, alizindua rasmi gazeti la kila wiki la Umoja Daima ambalo awali lilikuwa likitoka kama Jarida kila baada ya miezi mitatu.

Akizungumza katika kikao hicho Askofu Dkt. Shoo amewataka wakristo waishio nje ya Dayosisi kujitoa katika kuboresha taasisi mbalimbali za kimaendeleo zilizopo katika Dayosisi.

Alisema kuwa michango na ushauri unaotolewa na wanadayosisi waliopo safarini inasaidia katika kuendeleza shughuli mbalimbali za kimaendeleo na kwamba ushauri wao umekuwa ukifanyiwa kazi katika kuboresha taasisi zilizopo.

Aidha aliwapongeza wanadayosisi walioko safarini kwani wamekuwa mfano mwema katika maeneo wanayoishi kwa kufanya kazi nzuri na kuwaeleza kuwa kufanya hivyo kunawaletea baraka za Mungu.

“Ninawaomba muendelea kumtumikia Mungu kwa kutoa huduma za kiroho na kimwili popote mlipo” Alisistiza Askofu Dkt. Shoo.

Kwa upande wa Wanadayosisi waliopo nje wamesema kuwa, kukutana kwao na Mkuu wa Dayosisi kumekuwa na manufaa kwani imekuwa ni sehemu mojawapo ya kupata taarifa zinazoendelea ndani ya Dayosisi yao.

Akihitimisha hotuba yake Askofu Shoo aliwataka Wanadayosisi popote watakapokuwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka 2024.

For to us a child is born, to us a child is given, and the government shall be on his shoulders. And he shall be called Wonderful Counselor, Mighty God, Everlasting Father, Prince of Peace. (Isaiah 9:6)

Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake nae ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, baba wa milele Mfalme wa amani. (Isaya 9:6)

Dkt. Kweka aliitwa mbinguni akiwa na umri wa miaka 89.

Wasifu

Askofu Dkt. Kweka alikuwa ni mtu mwenye kipawa cha uongozi tangu akiwa shule ya msingi. Alikuwa kiranja wa wanafunzi, kapteni wa timu ya mpira wa miguu na pia kiongozi katika bendi ya shule, ambayo ilitumbuiza katika siku kubwa ya Wachagga ya kumtunuku Mangi Mkuu.

Askofu Dkt. Kweka alionyesha umahiri mkubwa katika uongozi wa Kanisa na alitoa mchango mkubwa kwa jamii kulikomfanya atunukiwe shahada mbili za Udaktari wa Heshima (Shahada za Uzamivu) “Honoris Causa” kama ifuatavyo:

Baba yake alipofariki, mwaka 1948, yeye alikuwa na umri wa miaka 14 jambo lililomsababisha kubeba majukumu ya kutunza familia iliyokuwa na Mama mzazi, Babu na Bibi pamoja na ndugu zake saba. Akiwa mvulana wa umri mdogo yeye pamoja na wavulana wengine, walianzisha biashara ndogo ya kuuza matunda na mayai ya kuchemsha katika kambi za jeshi zilizokuwapo eneo la Mailisita, Weruweru, kwa lengo la kujipatia kipato.

Akiwa Mwalimu alianzisha duka nyumbani kwa lengo la kujipatia kipato. Akiwa masomoni Makumira na Marekani alianzisha bustani ya mbogamboga alizoziuza na kujiongezea kipato cha kutunza familia. Tabia yake ya kufanya shughuli za kujiongezea kipato na kujitegemea aliendelea nayo katika maisha yake yote ya utumishi na hata baada ya kustaafu. Tabia hii ya kufanya kazi kwa bidii na kujitegemea aliisisitiza kwa jamii na kwa wachungaji. Katika uongozi wake aliitenga siku ya Jumatatu kwa wachungaji ili waweze kufanya shughuli za maendeleo ya kiuchumi na uzalishaji katika familia ili kuongeza kipato chao na kujitegemea.

Askofu Dkt. Kweka alikuwa mtu mwenye msimamo thabiti kwenye ukweli hata kama msimamo huo ungetishia usalama wake.

Askofu Dkt. Kweka, alikuwa mtu mwenye kupenda amani na msuluhishi wa migogoro mbalimbali. Alikuwa ni mtu mwenye upendo, mwenye kujali na mwepesi kusamehe. Alikuwa ni baba aliyeipenda sana familia yake na kuitunza.

Askofu Dkt. Kweka alipenda sana kusoma vitabu mbalimbali, kutunza kumbukumbu na kuandika. Siku za mwisho za uhai wake alikabidhi uongozi wa Dayosisi kitabu alichoandika kinachoeleza kuhusu “Historia ya Vituo vya Dayosisi” na hii itabaki kuwa hazina kubwa kwa Dayosisi na vizazi vijavyo.

Shukrani

Tunamshukuru Mungu kwa maisha ya mtumishi wake Baba Askofu Dkt. Erasto N. Kweka.

Tunaishukuru familia yake hususan mkewe na watoto kwa kumsaidia katika utumishi wake katika Dayosisi, Kanisa na jamii kwa ujumla.

Tunawashukuru madaktari, wauguzi na wataalamu wengine wengi waliohusika kwa namna moja ama nyingine kumhudumia katika hali ya ugonjwa.

Tunaushukuru uongozi wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani kwa jinsi walivyojitoa kwa moyo wa upendo na undugu wa Kikristo kumhudumia kiroho na kimwili akiwa Hospitali ya Muhimbili – Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na kuifariji familia tangu kifo kilipotokea na kuratibu Ibada ya kuuaga mwili wake Kanisa Kuu, Azania Front pamoja na kuusindikiza mwili wake kuja Moshi.

Tunawashukuru viongozi wa Kanisa, jamii na watu wote walioshirikiana na familia na Dayosisi katika kuuguza, faraja wakati wote wa msiba, na siku ya leo kumlaza Baba Askofu.

“Kwa maana Daudi, akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala, akawekwa pamoja na baba zake….” ( Mdo. 13:36a)

Warsha ya Mpango Mkakati wa Dayosisi 2024-2028 ya Maofisa wa Dayosisi, Wadiri (Wakuu wa Idara), Wakuu wa Majimbo na Vituo vya Elimu, Uchumi, Afya na Huduma imefanyika imefanyika  Uhuru Lutheran Hotel & Conference leo tarehe 16/11/2023.

Katika mpango huo kuna vipaombele 5 ambavyo ni pamoja na:

  1. Kuwa na ukuaji Endelevu
  2. Kuwa na ukuaji endelevu wa Kifedha na Kiuchumi
  3. Kuwa na Utawala Bora na Ufanisi wa Kiutendaji
  4. Kuwa na Huduma za Kijamii zilizo bora na zenye usawa
  5. Kuwa na Haki za Kimazingira, Kijamii, Kiuchumi na

Askofu Dkt. Shoo amstaafisha Mch. Leonard Kessy Usharika wa Wiri

Ofisi yafunguliwa Lengongu

Tuitikie Wito kwa Moyo Mnyofu

Mkuu wa KKKT na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, ameongoza Ibada ya kumstaafisha kwa heshima Mch. Leonard Kessy, Ibada iliyofanyika katika Usharika wa Wiri mtaa wa Ebenezer Jimbo la Siha Oktoba 22, 2023.

Ibada hiyo ilitanguliwa na ufunguzi wa Ofisi ya Mtaa wa Lengongu iliyogharimu kiasi cha shilingi milioni 92, fedha zilizochangwa na washarika. Tendo hilo lilifanywa na Askofu Dkt. Fredrick Shoo akishirikiana na Msaidizi wa  Askofu Mch. Deogratius Msanya na Mkuu wa Jimbo la Siha Mch. Elisa Kileo.

Katika ibada hiyo Askofu Dkt. Shoo alimpongeza Mch. Kessy kwa kustaafu kwa heshima na kusema kuwa ni jambo la kumshukuru Mungu pale mtumishi anapomaliza wito wa utumishi wake salama. Pia alipongeza Usharika kwa maono mazuri ya ujenzi wa Ofisi ya Kisasa yenye ukumbi wa mikutano na chumba cha kulala cha watumishi wageni.

Mch. Leonard Kessy alianza huduma ya Uchungaji mwaka 1990 na alitumika katika sharika za Makivaru Meru mwaka 1990-1992, Naibili mwaka 1993-1998, Wiri mwaka 1999-2005, Olmolog 2006, Ngaritati na Wiri 2006-2009, Ivaeny  2010-2021 na Usharika wa Nasai Oktoba 2021-2022. Mchungaji ametumika kwa miaka 32.

Akihubiri katika ibada hiyo Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya aliwataka Watumishi na Wakristo kwa ujumla kutii wito kwa kugeuka na kuacha maovu. Alisema Mungu anatuita kutoka katika njia zisizofaa na kuwa wasafi ndipo tukatumikie wito aliotuitia.

Mahafali ya 70 Yafanyika Mwika, 70 Wahitimu,

Mch. Overa Suhlberg Astaafu kwa Heshima,

Atumika miaka 31.

Askofu Dkt. Shoo Awataka wahitimu Kutumika kwa Uaminifu

Mkuu wa KKKT na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo ametoa vyeti kwa wahitimu 70 katika mahafali ya 70 ya Chuo cha Biblia na Theologia Mwika Oktoba 20, 2023.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Chuo cha Biblia na Theologia Mwika Mch. Obed Akyoo alisema, wahitimu waliothibitishwa kuhitimu katika kozi mbalimbali ni pamoja na wahitimu 37 wa kozi ya Elimu ya Kikristo na Uinjilisti ngazi ya cheti, 14 wamehitimu kozi ya Wasaidizi wa Sharika Huduma za Jamii ngazi ya cheti, 10 kozi ya muziki wa Kanisa ngazi ya cheti. Wengine ni 3 Kozi ya Muziki ngazi ya Stashahada na 6 walihitimu kozi ya Theologia ngazi ya Cheti.

Kabla ya kuwatunuku vyeti wahitimu hao Askofu Dkt. Shoo aliwataka wahitimu hao kwenda kwenye utumishi na huduma waliyoitiwa na  Mungu na kutumika kwa uaminifu wakitambua nguvu yao itatoka kwa Yesu pekee.

Alisema wawapende wale watakaowahudumia na kuwahudumia kwa bidii na kwa uaminifu bila ubaguzi kama wafuasi wa Yesu Kristo. “Msiende kufanya mambo ya usanii kama wanaofanya baadhi ya watumishi” Aliwataadharisha Askofu Dkt. Shoo

Mchungaji Overa Suhlberg Astaafishwa kwa Heshima.

Katika ibada hiyo ya mahafali ya 70, Mkuu wa Kanisa na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Shoo alimstaafisha kwa heshima Mchungaji Overa Suhlberg baada ya kutumika katika huduma ya kichungaji kwa miaka 31.

Mchungaji Overa alianza huduma ya kichungaji mwaka 1992 ambapo alitumika katika kanisa la Kulutheri nchini Sweden mwaka 1992-2013. Baada ya kutumika Nchini Sweden mwaka 2014 hadi anastaafu alikuwa Mkufunzi wa Chuo cha Biblia na Theologia Mwika.

Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya ameongoza Ibada ya Sikukuu ya Vijana na Uimbaji katika ngazi ya Dayosisi iliyofanyika katika Usharika wa Himo Jimbo la Kilimanjaro Mashariki Oktoba 15, 2023 ambapo kwaya 24 zilishiriki sikukuu ya vijana na uimbaji.

Kwaya hizo ni kutoka katika Sharika na Vituo mbalimbali katika  majimbo 5 ya Dayosisi baada ya kufuzu kushiriki uimbaji katika ngazi ya sharika kanda na majimbo. Siku hii ya uimbaji katika ngazi ya Dayosisi hufanyika kila mwaka na huratibiwa na Halmashauri ya Liturugia na Uimbaji ya Dayosisi.

Akifungua mashindano hayo Msaidizi wa Askofu Mch. Deogratius Msanya alisema waimbaji wanapaswa kutambua kuwa ili kumsifu Mungu kwa uzuri  inafaa kuimba wakiwa na Mioyo Minyofu. Alisema moyo mnyoofu ni mojawapo ya kanuni ya msingi ya kuzingatia katika kumsifu Mungu ukiacha kanuni ya kitaalamu.

Aidha alisema kuwa, kuimba kitaalamu ni kanuni nzuri ya kumsifu Mungu kwa uzuri lakini pasipo kuzingatia kanuni ya Unyofu wa Moyo kuimba au kusifu kwetu kunabadilika na kuwa kelele mbele za Mungu. Alihimiza kuwa tunapokosea kanuni ya unyoofu wa Moyo tunaathiri kanuni namba moja ya utaalamu katika kusifu

“Uzuri wa kumsifu Mungu ni kumsifu katika utakatifu, katika hali ya usafi. Tunapaswa kujitenga na uchafu na machukizo mbele za Mungu; waimbaji mnapaswa kumsifu Mungu katika usafi, angalieni Zaburi ya 33:1 wa kwanza inavyotukumbusha”.Alieleza Mch. Msanya.

Naye katibu wa Idara ya Vijana wanafunzi anayeratibu uimbaji Dayosisi Mch. Mathayo Mtui amesema Sikukuu ya Dayosisi imejejipanga kufanya matamasha na semina mbalimbali kwa vikundi mbalimbali kwa lengo la kuimarisha  kwaya ili ziweze kutunga na kuimba nyimbo zenye kumsifu na kumtukuza Mungu.

Kwa upande wa waimbaji walioshiriki katika uimbaji akiwemo mwimbaji wa kwaya ya wanaume Usharika  wa Himo  Bw. Edward Shayo  alisema kuwa kipindi cha nyuma wanaume walikuwa hawana ari ya ushiriki tofauti na sasa ambapo amesema ari hiyo  inatokana na kuona faida ya kumwimbia Mungu.

Matokeo ya washiriki

Katika Uimbaji huo kundi la kwanza la Sekondari Mchanganyiko, nafasi ya kwanza ilishikwa na Shule ya Seminari Agape kwa alama 88 ikifuatiwa na mshiriki mwezake shule ya Sekondari Kilimatembo mwenye alama 80.

Kundi la pili lilikuwa la Sekondari Wavulana na nafasi ya kwanza ilishikwa na Shule ya Sekondari ya Wavulana Lyamungo kwa alama 76. Vilevile kundi la tatu la Vyuo Mchanganyiko Chuo Cha Biblia na Theologia mwika walishika nafasi ya kwanza kwa alama 83 ambapo pia hawakuwa na mpinzani.

Kwa kundi la nne la Kwaya za tarumbeta jumla ya kwaya zilizoshiriki zilikuwa 5. Nafasi ya kwanza ilishikwa na kwaya ya Usharika wa Sanya Juu na Uuwo kwa kufungana kwa alama 81, nafasi ya pili Usharika wa Hai kwa alama 82, nafasi ya tatu kwaya ya Karatu Mjini kwa alama 72 na nafasi ya tano ilishikwa na kwaya ya Usharika wa Moshi Mjini kwa alama 66.

Kundi la tano lilikuwa Kwaya ya Wanaume ambapo kwaya 5 zilishiriki. Nafasi ya kwanza iliongozwa na Usharika wa Himo kwa kupata alama 87 ikifuatiwa na kwaya ya Moshi Mjini kwa alama 86. Nafasi ya tatu kwaya ya Shiri kwa alama 82, nafasi ya nne kwaya ya Karansi kwa alama 80 na nafasi ya tano kwaya ya Karatu Mjini kwa alama 69.

Vilevile kundi la sita lilikuwa la Kwaya za Vijana Sharikani ambapo kwaya 5 zilishiriki. Katika kundi hili nafasi ya kwanza ilishikwa na Usharika wa Upperkitete kutoka Karatu kwa alama 85, ya pili Usharika wa Kingereka kwa alama 83. Nafasi ya 3 katika kundi hili ilishikwa na kwaya Himo kwa alama 76, ya nne Majengo alama 73 na nafasi ya tano Usharika wa Orkolili kwa alama 69.

Kundi la 7 lilikuwa Kwaya za Mchanganyiko Shariani, kundi hili pia lilikuwa na kwa tano. Nafasi ya kwanza kwa kundi hili iliongozwa na kwaya ya Usharika wa Kiboriloni kwa alama 89, ya pili Usharika wa Lyamungo Kati alama 85, ya tatu Usharika wa Lole kwa alama 83 na nafasi ya nne kwaya mbili za Usharika wa Sanya Juu na Rhotia zilifungana kwa alama 79.

Wataalamu walioshiriki katika kushauri pamoja na kutoa alama ni pamoja na Mch. Herzon Mashauri kutoka Dayosisi ya Kaskazini Kati, Mwalimu Loi Kisiri kutoka Dayosisi ya Meru na Mwalimu David Mwera kutoka Anglikana Arusha.

Mkutano Mkuu wa 16 wa Jimbo la Hai umefanyika Oktoba 11, 2023 katika bustani ya Jimbo ambapo ulifunguliwa rasmi na Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania na Dayosisi ya Kaskazini, Askofu Dkt. Fredrick Oanel Shoo. Katika mkutano huo taarifa ya jimbo ilitolewa  na Mkuu wa Jimbo na kujadiliwa na wajumbe toka sharika zote za Jimbo kisha kuweka maazimio na mipango mbalimbali ya Jimbo.

Mkutano huo uliambatana na  uwekaji wa jiwe la pembe kituo cha kutwa cha malezi ya watoto (Day care) tendo lililoongozwa na Mkuu wa Kanisa ambapo Katibu wa Jimbo Mwinjilisti Erinest Massawe alisema kuwa, wazo la ujenzi wa kituo hicho ni kuonekana kuwepo kwa uhitaji wa vituo hivyo kutokana na idadi ya watu na watoto kuongezeka.

Akifundisha neno kuu la mkutano Askofu Dkt. Shoo  alisema kuwa umoja na ushirikiano ni jambo la msingi na lakuzingatia katika kujenga mwili wa Kristo  yaani Kanisa.

Askofu Shoo amesema hayo wakati alipokuwa akifungua mkutano Mkuu wa 16 wa Jimbo hai Dayosisi  ya Kaskazini iliyofanyika jimboni hapo mkoani Kilimanjaro.

Alisema  ndani ya mwili wa Kristo Kuna vipawa na karama nyingi ambavyo vikitumika kwa umoja bila ubinafsi kuna kuwa na ufanisi katika utendaji kazi kwenye Sharikani, Jimbo  na  Kanisa kwa ujumla.

Sambamba na hayo alisema kuwa semu ambayo ilitakiwa kujengwa mwili wa Kristo imegeuka na kuwa  sehemu ya mafarakano kutokana na kutokutambua kwamba karama zote zinatoka kwa Mungu na tunazipata kwa Neema tu.

Kwa upande wake Katibu wa Dayosisi ya Kaskazini Mhandisi Z.S Moshi amewataka viongozi mbalimbali wa Jimbo kunia pamoja na kufanya kazi kwa pamoja na kuweka ubinafsi pembeni.

Naye Mkuu wa Jimbo la Hai mchungaji Biniel Mallyo alisema kuwa Jimbo la Hai limefanikiwa katika nyanja mbalimbali ambapo amewataka watumishi wa Jimbo kudumisha utulivu waweze kufanya kazi ya Mungu kwa furaha.

Mkuu wa Kanisa na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo, ameongoza ibada ya kumstaafisha kwa heshima Parish worker Isaria Noel Lema wa Usharika wa Nronga Jimbo la Hai la KKKT Dayosisi ya Kaskazini Oktoba 8, 2023. Ibada hiyo iliambatana na maadhimisho ya sikukuu ya Mikaeli na watoto.

Parish worker Isaria Lema ametumika katika shamba la Bwana kwa takribani miaka 37 hadi anastaafu. Historia yake inaeleza kuwa Isaria Noel Lema alisoma Uinjilisti katika Chuo cha Biblia na Theologia Mwika mwaka 1981-1982.  Mwaka 1983 alihudumu katika Usharika wa Kawaya kama Mwinjilisti na Parish worker kabla ya kwenda kwenye masomo rasmi ya Parish worker katika Chuo cha Biblia na Theologia Mwika mwaka 1984-1985.

Baada ya kuhitimu masomo hayo mwaka 1986 alihudumu kama Parish worker katika Usharika wa Nronga pamoja na kufundisha Elimu ya Dini katika shule za msingi na masomo ya ufundi cherehani, shule ya Jumapili n.k hadi alipostaafu kwa heshima Oktoba 8, 2023.

Awali Mkuu wa Kanisa na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo alimpongeza kwa utumishi wake ambapo alieleza kuwa amefanya kazi kubwa ya kuwafundisha watoto kufahamu msingi wa neno la Mungu utakaowasaidia kuwa nuru katika familia, jamii, Kanisa na Taifa.

Alisema watoto wanapopewa mafundisho yatakayowasaidia kuwaongoza kukua katika njia inayopasa kwa kuzingatia msingi wa neno la Mungu wanakuwa baraka katika familia na jamii kwa ujumla.

Naye Mkuu wa Jimbo la Hai Mch. Biniel Mallyo akihubiri katika ibada hiyo alisema tunapaswa kutumia wakati tuliopewa na Mungu ipasavyo katika kuifanya kazi yake kutimiza kusudi lake aliloweka kwa kila mwanadamu.

Alisema wanadamu wanapaswa kutambua kuwa Mungu ana kusudi au lengo la kumleta hapa duniani hivyo kuna haja ya kufahamu kusudi hilo na kulitimiza.

Alisema wazazi na walezi wana wajibu wa kuwasaidia watoto wao kufahamu kusudi/lengo la wao kuwepo hapa duniani ili waweze kulitimiza.

“Ni muhimu kuwaandaa watoto mara wanapokuja hapa duniani kutambua kusudi/lengo la wao kuwepo duniani, maana wanapotambua wataweza kutenda yaliyo mema na kuiweka jamii na taifa katika mstari mwema”. Alisema Mch. Mallyo.

Alihitimisha kwa kuhimiza kufanya kazi kwa bidii ikiwa bado mapema na tukiwa na nguvu kama neno la Mungu linavyotuasa kufanya kazi kwa bidii angali bado mchana akinukuu neno linavyotufundisha kuwa…  ‘Imetupasa kuzifanya kazi zake yeye aliyenipeleka maadamu ni mchana, usiku waja aspoweza mtu kufanyakazi” (Yohana 9:4).

Akitoa salam za pongezi kwa Parishwoker Lema; Mkuu wa Wilaya ya Hai Mhe. Amir Mohamed Mkalipa alimpongeza Mkuu wa Kanisa kwa jinsi anavyoweka mkazo mkubwa katika malezi ya watoto.

“Nimeshuhudia hapa jinsi watoto walivyoonyesha ukomavu katika mafundisho ya neno la Mungu na maadili kwa ujumla kupitia mashairi, ngojera na maigizo. Wamechukua sehemu kubwa ya hotuba yangu, wametuasa masuala ya ulevi na malezi kwa wazazi. Nampongeza mama yetu Lema kwa kazi nzuri aliyoifanya kwa watoto hawa”. Alisema Mhe. Mkalipa.

Katika ibada hiyo watoto wa shule ya Jumapili walisheherekea sikukuu yao ya Mikaeli na watoto ambayo ilipaswa kufanyika Jumapili iliyopita lakini kwa heshima ya kumuaga mwalimu wao walisheherekea pamoja naye katika siku yake ya kustaafu.

Katika ujumbe wao kwa wazazi waliwaomba kuwajali, kuwalinda, kuwapa Elimu bora, kuwa na muda wa kukaa na familia na kuacha ulevi.

Kwa upande wake Parish Worker Lema aliwashukuru wote walioshirikiana naye katika utumishi wake. Pia aliwaomba wale wanaobaki katika kazi kuendelea kushirikiana, kupendana na kufanya kazi kwa umoja ili kazi ya Mungu isonge mbele.

Katibu wa Leipzig Mission Tanzania kutoka Ujerumani Mchungaji Dkt. Daniel Keiling ametembelea Makao makuu ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini leo asubihi Septemba 27,2023.

Kwenye Picha aliyevaa koti ni Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Mhandisi Z.S. Moshi akipokea zawadi iliyotolewa na Mchungaji Daniel mwenye shati jeusi na kola nyeupe ya Kichungaji.