Mkuu wa KKKT na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo aliongoza kikao cha Wanadayosisi waliopo Safarini (Diaspora) Disemba 27, 2023 Uhuru Lutheran Hotel& Conference Centre kikao ambacho hufanyika kila mwisho wa mwaka kujadili masuala mbalimbali yahusuyo maendeleo ya Dayosisi.
Sambamba na kikao hicho, alizindua rasmi gazeti la kila wiki la Umoja Daima ambalo awali lilikuwa likitoka kama Jarida kila baada ya miezi mitatu.
Akizungumza katika kikao hicho Askofu Dkt. Shoo amewataka wakristo waishio nje ya Dayosisi kujitoa katika kuboresha taasisi mbalimbali za kimaendeleo zilizopo katika Dayosisi.
Alisema kuwa michango na ushauri unaotolewa na wanadayosisi waliopo safarini inasaidia katika kuendeleza shughuli mbalimbali za kimaendeleo na kwamba ushauri wao umekuwa ukifanyiwa kazi katika kuboresha taasisi zilizopo.
Aidha aliwapongeza wanadayosisi walioko safarini kwani wamekuwa mfano mwema katika maeneo wanayoishi kwa kufanya kazi nzuri na kuwaeleza kuwa kufanya hivyo kunawaletea baraka za Mungu.
“Ninawaomba muendelea kumtumikia Mungu kwa kutoa huduma za kiroho na kimwili popote mlipo” Alisistiza Askofu Dkt. Shoo.
Kwa upande wa Wanadayosisi waliopo nje wamesema kuwa, kukutana kwao na Mkuu wa Dayosisi kumekuwa na manufaa kwani imekuwa ni sehemu mojawapo ya kupata taarifa zinazoendelea ndani ya Dayosisi yao.
Akihitimisha hotuba yake Askofu Shoo aliwataka Wanadayosisi popote watakapokuwa kushiriki kikamilifu katika uchaguzi mdogo wa serikali za mitaa utakaofanyika mwaka 2024.
For to us a child is born, to us a child is given, and the government shall be on his shoulders. And he shall be called Wonderful Counselor, Mighty God, Everlasting Father, Prince of Peace. (Isaiah 9:6)
Maana kwa ajili yetu mtoto amezaliwa, tumepewa mtoto mwanamume; Na uweza wa kifalme utakuwa begani mwake nae ataitwa jina lake, Mshauri wa ajabu, Mungu mwenye nguvu, baba wa milele Mfalme wa amani. (Isaya 9:6)


Dkt. Kweka aliitwa mbinguni akiwa na umri wa miaka 89.
Wasifu
Askofu Dkt. Kweka alikuwa ni mtu mwenye kipawa cha uongozi tangu akiwa shule ya msingi. Alikuwa kiranja wa wanafunzi, kapteni wa timu ya mpira wa miguu na pia kiongozi katika bendi ya shule, ambayo ilitumbuiza katika siku kubwa ya Wachagga ya kumtunuku Mangi Mkuu.
Askofu Dkt. Kweka alionyesha umahiri mkubwa katika uongozi wa Kanisa na alitoa mchango mkubwa kwa jamii kulikomfanya atunukiwe shahada mbili za Udaktari wa Heshima (Shahada za Uzamivu) “Honoris Causa” kama ifuatavyo:
Baba yake alipofariki, mwaka 1948, yeye alikuwa na umri wa miaka 14 jambo lililomsababisha kubeba majukumu ya kutunza familia iliyokuwa na Mama mzazi, Babu na Bibi pamoja na ndugu zake saba. Akiwa mvulana wa umri mdogo yeye pamoja na wavulana wengine, walianzisha biashara ndogo ya kuuza matunda na mayai ya kuchemsha katika kambi za jeshi zilizokuwapo eneo la Mailisita, Weruweru, kwa lengo la kujipatia kipato.
Akiwa Mwalimu alianzisha duka nyumbani kwa lengo la kujipatia kipato. Akiwa masomoni Makumira na Marekani alianzisha bustani ya mbogamboga alizoziuza na kujiongezea kipato cha kutunza familia. Tabia yake ya kufanya shughuli za kujiongezea kipato na kujitegemea aliendelea nayo katika maisha yake yote ya utumishi na hata baada ya kustaafu. Tabia hii ya kufanya kazi kwa bidii na kujitegemea aliisisitiza kwa jamii na kwa wachungaji. Katika uongozi wake aliitenga siku ya Jumatatu kwa wachungaji ili waweze kufanya shughuli za maendeleo ya kiuchumi na uzalishaji katika familia ili kuongeza kipato chao na kujitegemea.
Askofu Dkt. Kweka alikuwa mtu mwenye msimamo thabiti kwenye ukweli hata kama msimamo huo ungetishia usalama wake.
Askofu Dkt. Kweka, alikuwa mtu mwenye kupenda amani na msuluhishi wa migogoro mbalimbali. Alikuwa ni mtu mwenye upendo, mwenye kujali na mwepesi kusamehe. Alikuwa ni baba aliyeipenda sana familia yake na kuitunza.
Askofu Dkt. Kweka alipenda sana kusoma vitabu mbalimbali, kutunza kumbukumbu na kuandika. Siku za mwisho za uhai wake alikabidhi uongozi wa Dayosisi kitabu alichoandika kinachoeleza kuhusu “Historia ya Vituo vya Dayosisi” na hii itabaki kuwa hazina kubwa kwa Dayosisi na vizazi vijavyo.
Shukrani
Tunamshukuru Mungu kwa maisha ya mtumishi wake Baba Askofu Dkt. Erasto N. Kweka.
Tunaishukuru familia yake hususan mkewe na watoto kwa kumsaidia katika utumishi wake katika Dayosisi, Kanisa na jamii kwa ujumla.
Tunawashukuru madaktari, wauguzi na wataalamu wengine wengi waliohusika kwa namna moja ama nyingine kumhudumia katika hali ya ugonjwa.
Tunaushukuru uongozi wa KKKT Dayosisi ya Mashariki na Pwani kwa jinsi walivyojitoa kwa moyo wa upendo na undugu wa Kikristo kumhudumia kiroho na kimwili akiwa Hospitali ya Muhimbili – Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete na kuifariji familia tangu kifo kilipotokea na kuratibu Ibada ya kuuaga mwili wake Kanisa Kuu, Azania Front pamoja na kuusindikiza mwili wake kuja Moshi.
Tunawashukuru viongozi wa Kanisa, jamii na watu wote walioshirikiana na familia na Dayosisi katika kuuguza, faraja wakati wote wa msiba, na siku ya leo kumlaza Baba Askofu.
“Kwa maana Daudi, akiisha kulitumikia shauri la Mungu katika kizazi chake, alilala, akawekwa pamoja na baba zake….” ( Mdo. 13:36a)
Ni tukio la kihistoria, ndivyo tunavyoweza kuandika, kwani ni baada ya takribani miaka ishirini kwa mujibu wa baadhi ya washiriki ambao ni wainjilisti kutoka katika Majimbo yote matano ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini!
Wainjilisti 384, kati yao wanawake 124 sawa na 34% na wanaume 260 sawa na 66% kutoka katika sharika 171 za KKKT Dayosisi ya Kaskazini, walikutana tarehe 6-9 Septemba, 2023 katika Chuo cha Biblia na Theolojia Mwika kwa semina ya siku tatu.
Semina hiyo iliratibiwa na Idara ya Misioni na Uinjilisti ya KKKT Dayosisi ya Kaskazini ambayo Mudiri wake ni Mhe. Msaidizi wa Ask. Mch. Deogratius Msanya. Semina hii ni sehemu ya mpango wa Dayosisi wa kuimarisha uinjilisti katika Dayosisi na kuwajengea uwezo wa utoaji taarifa, kuwapatia maarifa na ujuzi watumishi wa kada ya Uinjilisti katika Dayosisi. Aidha, ni fursa pia ya watumishi hawa kushiriki pamoja Neno la Mungu, kuomba, kuimba n.k
Ifahamikwe kwamba, katika kipaumbele cha uendelevu wa Kanisa katika Mpango Mkakati wa Dayosisi 2023-2027, Dayosisi imejiwekea malengo ya kukua kwa idadi ya washarika wapya zaidi ya 160,000 kwa kipindi cha miaka mitano. Kukua huku, kutatokea kupitia uinjilisti kwa kuwa na mikutano ya wazi, nyumba kwa nyumba, makundi maalumu, kadhalika kupitia majukwaa ya kidijitali hususan mitandao ya kijamii.
Akifungua semina hiyo, Mhe. Askofu Dkt. Shoo aliwapongeza wainjilisti kwa kupata fursa ya kukutana pamoja kwa lengo la kujengeana uwezo na kuimarishana katika huduma. Aliwaambia kuwa huduma yao imekuwa ya baraka na ni uti wa mgongo kwa Dayosisi na Kanisa kwa ujumla. Alisema kuwa, huduma yao katika ustawi wa Kanisa ni ya muhimu sana na kuwataka kuitumia fursa hiyo ya kukutana kujadilia mambo mbalimbali katika utumishi yatakayosaidia kujenga na kuendeleza Kanisa.
Akirejea somo la ufunguzi kutoka kitabu cha 2 Wakorintho 4:1-9 lisemalo, “Kwa sababu hiyo, kwa kuwa tuna huduma hii, kwa jinsi tulivyopata rehema, hatulegei; lakini tumekataa mambo ya aibu yaliyositirika……”
Ask. Dkt. Shoo alisema kwamba, ni muhimu na lazima kwa watumishi wa Kanisa kuzingatia sana neno lisemavyo; kuwa imara katika huduma na kufundisha kweli ya Neno la Mungu bila kulegea na kutambua kuwa huduma hii wamepewa kwa neema tu.
Aliendelea kusema,“Ninyi ni wahudumu wa zama hizi mpya na mmepewa kazi hii kwa rehema na kwa Neema ya Mungu; Neno la Mungu linawakumbusha msije mkajisahau kwamba mnastahili kuwa katika hii huduma, ni kwa neema tu. Mtumishi wa Mungu anapojisahau na kufikiri kwamba anastahili; Shetani anajiinua na kumpa kiburi na mwisho analegea katika huduma”.
Pia aliwataka watumishi hao kujihadhari sana na tabia ya kulichanganya Neno la Mungu na uongo. Alisema wanapaswa kulihubiri Neno la Mungu katika usafi na usahihi wake ili watu wa
Mungu waimarishwe kiimani kwa taarifa na maarifa sahihi kuhusu Neno la Mungu na maisha ya ufuasi hususan kwa kuzingatia tafsiri na mikazo ya Kilutheri. “Mafundisho ya utajirisho yanapotosha ukweli wa Neno la Mungu. Badala ya kufundisha watukufanya kazi kwa bidii, baadhi ya watumishi wanawafundisha kupokea tu katika ndoto bila kuwaelekeza watu kufanya kazi kwa bidii huku wakimwomba na kumtegemea Mungu.”
Mhe. Ask. Dkt. Shoo alihitimisha hotuba yake kwa kusisitiza wainjilisti ,kutafakari mafundisho yanayofundishwa na kutambua yanalenga wapi . “Wakristo wengi wamerudi kule walipokuwepo wazee wetu kabla ya Ukristo, wanapewa maji, vitambaa, mafuta n.k., huu ni kama ushirikina. Fundisheni, onyeni watu ili waweze kulifahamu Neno la Mungu na ukweli wake wote ili waweze kuepuka mafundisho potofu”. Alisema Dkt. Shoo.
Naye Mwinjilisti Kaveja kwa niaba ya Wainjilisti wote, alimshukuru sana Ask. Shoo kwa mafundisho na nasaha alizowapa na alishukuru Dayosisi kuandaa semina hiyo muhimu na alimpongeza kwa jitihada zake za dhati za kusimamia Injili katika Kanisa. Alisema, “Sisi Wainjilisti tunakushukuru sana kwa kutupa fursa hii ya kukutana pamoja, jambo ambalo halikufanyika kwa takribani miaka 20.” kauli ambayo ilisindikizwa kwa makofi mengi kutoka kwa washiriki.
Aidha, Mwinjilisti Kaveja, alihitimisha kwa kusema, “Tumefurahi na tumeguswa na maono ya Dayosisi ya kuwezesha semina hii. Sisi kama Wainjilisti tutatekeleza kwa uaminifu yale yote uliyoelekeza na kuasa. Tutayafanyia kazi na kuwa na subira kwa yale mazuri yaliyopangwa kwa ajili yetu”, alihitimisha.
Ibada ya ufunguzi wa Mkutano Mkuu wa 13 wa Fungamano la Makanisa ya Kilutheri Duniani (LWF) ikiendelea katika mji wa Krakow-Poland ambapo baadhi ya viongozi kutoka KKKT wameshiriki akiwepo Mkuu wa Kanisa Askofu Dkt. Fredrick Shoo, Askofu Dkt. Mbilu, Katbu Mkuu wa KKKT Mhandisi Robert Kitundu n.k

Semina ya watetezi haki za jinsia imefanyika Agosti 30, 2023 katika ukumbi wa mikutano Umoja Lutheran Hostel Moshi Mkoani Kilimanjaro ikihusisha maeneo mbalimbali ya vijiji katika wilaya za Hai, Siha, Moshi Vijijini na Rombo.
Semina hiyo imewezeshwa na KKKT Dayosisi ya Kaskazini wakishirikiana na Dawati la Utetezi kutoka Makao Makuu ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania. Mradi huo unatekelezwa pia katika Dayosisi ya Mbulu-Manyara, Dayosisi ya Kati-Singida na Dayosisi ya Kaskazini Kati-Arusha.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Dawati la Utetezi KKKT Bibi. Besetina Saikong amesema lengo la semina hiyo ni kutoka Elimu ya kuondoa ukatili katika jamii ufahamu kuhusu migogoro.
Awali akifundisha mada kuhusu migogoro na utatuzi wa migogoro Bibi. Saikong alisema migogoro ni misuguano au kutokuelewana baina ya pande mbili mfano mtu na mtu, kikundi na kikundi n.k.
Alisema migogoro inasababisha kukosekana kwa amani na hata kuzorotesha shughuli mbalimbali za kimaendeleo kuanzia ngazi ya familia hadi taifa.
Alitaja mambo mbalimbali yanayoweza kusababisha migogoro kuwa ni pamoja na masuala ya kiuchumi, kisiasa,. umiliki wa raslimali, mahusiano na ukosefu wa Elimu au uelewa kuhusu jambo linaloweza kusababisha mgogoro.
Sababu nyingine alisema ni kukosekana kwa utawala bora na utawala wa sheria, mila na tamaduni zetu, ufinyo na uwiano usio sawa wa mgawanyo wa raslimali, ukiukwaji wa haki za binadamu, ukabila, ubaguzi, kukosekana kwa maadili katika jamii, kukosekana kwa mahitaji muhimu kama maji, barabara, shule na kukosekana kwa taarifa muhimu na takwimu.
Kwa upande wake Katibu wa Idara ya Wanawake na Watoto wa KKKT Dayosisi ya Kaskazini Mch. Faustine Kahwa akifundisha Mada ya pili kuhusu ukatili na Athari zake alisema watetezi hao wa haki wanapaswa kujituma kwa bidii katika kazi wanayoifanya ya utetezi kuweza kutokomeza ukatili katika jamii.
Alisema wanapaswa kuwa mfano kuanzia nyumbani hadi katika maeneo yao ya kazi katika kuondoa na kupinga ukatili kwa nguvu zote”Wewe kama Mama au Baba pale nyumbani kwako, anzia hapo kuondoa ukatili maana inawezekana ukawa mtetezi lakini pale nyumbani ukawa unafanya vitendo vya kikatili katika familia” Alisema Mch. Kahwa.
Mch. Kahwa aliwatia moyo watetezi hao katika kuifanya kazi hiyo na kuwataka kutokata tamaa hata pale wanapokutana na vikwazo.
“Niwaombe mkafanye Kazi, wasilianeni na wachungaji, mashehe kuzungumzia vitendo vya kikatili pale mnapovibaini na hata mkikwamishwa mahali nendeni ngazi inayofuata na tumieni mbinu mbalimbali”. Alisema Mch. Kahwa.
Katika mada yake alitaja baadhi ya aina za ukatili wa kijinsia kuwa ni pamoja na Ukatili wa kimwili, Ukatili wa kisaikolojia, Ukatili wa kingono, Ukatili wa kiuchumi na Ukatili wa kiafya
Naye mmoja wa watetezi Haki Bibi. Amphorence Zakayo Mlay Kutoka kijiji cha Kahe alisema ukatili upo wa aina mbalimbali na anakutana na kesi nyingi za ukatili katika kijiji chak. Anasema kamati ya utetezi wamekuwa wakiendelea kutoka Elimu Katika maeneo mbalimbali kama misikitini, kanisani na hata siku za masoko kupunguza kasi ya vitendo vy kikatili.
“Juzi kimetokea kitendo cha kikatili sana hapa Kahe, mtoto wa miaka 2 aliokotwa umbali mrefu kutoka nyumbani anapoishi, umbali ambao mtoto huyo asingeweza kufika mwenyewe na aliokotwa akiwa ameshafariki pembezoni mwa mtaro na walipochunguza walibaini alilawitiwa na kesi hii tunaifatilia hivyo jamii watambue kweli vitendo vya kikatili ni vingi wasivifumbie macho” Alitoa ushuhuda Bibi. Mlay kuwa huo ni mfano wa vitendo vya kikatili wanavyokumbana navyo katika maeneo mbalimbali wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao.

Mkuu wa Jimbo la Kilimanjaro Mashariki Mch. Calvin Koola ameongoza Ibada ya uzinduzi wa maadhumisho ya Miaka 50 tangu kuanzishwa kwa Sharika za Rombo, ambapo uzinduzi huo ulifanywa katika Usharika wa Rongai Agosti 20, 2023
Awali akihubiri katika ibada hiyo, Mch. Koola alimshukuru Mungu kwa sharika hizo kufikisha miaka 50 ukanda wa Rombo.
Mch. Koola alitoa rai kwa wachungaji na wainjilisti kuhubiri injili kwa watu na kufanya uinjilisti wa nyumba kwa nyumba ili Sharika zikue na kuzaliwa Sharika nyingine zaidi.
Kuzaliwa kwa Sharika za Rombo
Kwa mujibu wa Risala iliyosomwa na Mch. Mstaafu Dkt. Eliasi Silayo alisema nuru ya injili iliangazia eneo la Rombo kutoka Usharika wa Mwika kati ya mwaka 1954 chini ya uongozi wa Hayati Mch :Kalebi Mangesho. Mahali pa kwanza kabisa kufikiwa injili Rombo ni Mtaa wa Nanjara. Mwinjilisti wa kwanza aliyeachwa kuendeleza kazi ya injili Rombo pamoja na changamoto mbalimbali walizokutana nazo.
Ni Mwinjilisti Eliamlisi Shao kutoka Lole baadae walifuata Wainjisti Aminieli Shao, Amilieli Urio, Mwinjilisti Joseph Silayo Kutoka Nanjara ambaye ni Mwinjilisti wa kwanza mwenyeji pia Mwinjilisti Aminieli Makyao.
Kazi ilipopanuka ulianzishwa mtaa wa Mashati Momwe mwaka 1959 baadae ulianzishwa mtaa wa Rongai mwaka 1963 mtaa huu wa Rongai ulitunzwa na mwinjilisti Danieli Makule kutoka Mamba Kokirie. Mtaa wa Kamwanga ulianzishwa kati ya mwaka 1997 na aliyekabidhiwa kutunza mtaa huo ni Mwinjilisti Penieli Shao Kutoka Lole hadi mwaka 1972 alipokabidhiwa Mwinjilisti Jastini Tarimo kutoka Nanjara ambaye ni Mwinjilisti wa pili mwenyeji.
Mwaka wa 1967 hadi 1974 mitaa hii minne iliongonzwa na kusimamiwa na Mwinjilisti Aminieli Makyao kutoka Mwika Mongai ambaye alipewa leseni maalumu iliyo mwezesha kufanya huduma maalumu za kichungaji kama kubatiza, chakula cha bwana, kupokea wakristo kundini n.k. pia alikuwa kiongozi wa wainjilisti wote Rombo.
Baada ya kazi kuendelea kupanuka Dayosisi iliamua Mitaa iliyopo Rombo iondolewe kuwa misioni ya Usharika wa Mwika na kuwa Misioni ya Dayosisi. Hivyo Mitaa hiyo minne yaani Nanjara, Mashati-Momwe, Rongai, na Kamwanga ikazinduliwa kuwa Usharika wa Rombo mnamo tarehe 04/08/1974 na kukabidhiwa Mchungaji kiongozi wa kwanza Mch: Elias. E. Silayo.
Baada ya usharika huu mpya kuzaliwa mwezi October 1974 ulifanikiwa kununuliwa eneo jipya na kufungua mtaa wa Tarakea mwezi Disemba mwaka 1974 na ukafunguliwa Mtaa mpya wa Mkuu.
Wakristo waliabudia kwenye Jengo lililokuwa la Mahakama ya Wilaya eneo la Ubaa Mwaka 1975 kwa kushirikiana na Mkuu wa Wilaya aliyekuepo kwa kipindi hicho walifanikiwa kupata eneo lenye hekari nne lililopo makao makuu ya Wilaya ambapo walifanikiwa kujenga Kanisa, nyumba ya Mchungaji na Hostel.
Ujenzi huo ulipata ufadhili kutoka Ujerumani ambao hayati Askoful Dkt. Stefano Rubeni Moshi aliwapatia Mwaka 1976 kabla hajafariki. Baada ya kufariki kazi hiyo na mahusiano hayo yaliendelezwa na Askofu Dkt. Erasto Kweka hadi ujenzi ulipokamilika mwaka 1983.
Mwaka 1977 ulianzishwa Mtaa wa Useri. Mwaka 1977 mpaka wa Kenya na Tanzania ulifungwa na wakristo wa Kenya waliokuwa wakiabudu Tarakea na Rongai walishindwa kufika kanisani Tanzania, Ikabidi waanzishe Mtaa wao unaoitwa Rongai Kenya eneo la Kariangei ambao sasa ni Usharika wa Loitokitoki Kenya. Mwaka 1978 ulianzishwa mtaa wa Emoritoti na baadaye Orkaswa.
Mwaka 1982 usharika wa Rongai ulianzishwa chini ya Shemasi Joseph Silayo na mwaka 1987 usharika wa Mkuu ulianzishwa chini ya hayati Mch Abide Kanango.
Mnamo mwaka 1993 Usharika wa Imortoti ulianzishwa kutoka usharika wa Rongai na Kiongozi wa kwanza akiwa Mch: Dauson Kaaya.
Kufikia mwaka 2002 Usharika wa Tarakea ulianzishwa kutoka Usharika wa Nanjara Mch: kiongzi akiwa ni Mch: Nelson Machange.
Mpaka sasa Sharika zote za Rombo kuanzia mwaka 1974 hadi leo ni Sharika Tano ambazo zinamitaa 24 ukiondoa Usharika wa Emortoti ambao umehamishiwa Jimbo la Sihaa. Eneo la Rombo ambalo ni Wilaya nzima yenye Tarafa 5, Kata 28, Vijiji 68 na Vitongoji 318 kuna Sharika nne na Mitaa 20 tu.
Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania na Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt. Fredrick Onael Shoo alifungua semina ya Wasaidizi wa Sharika (Parishworkers) ya Siku 3 iliyofanyika Katika kituo cha Wanawake Angaza Agosti 17-19, 2023.
Akizungumza na Parish workers (PW) hao, Askofu Dkt. Shoo aliwataka kujiamini na kutokuwa na mashaka wanapofanya kazi ya Mungu kwani huduma wanayofanya ni Muhimu katika Kanisa.
Alisema wasaidizi wa Sharika ni sehemu muhimu sana Katika kanisa la Bwana na Dayosisi inatambua thamani ya huduma yenu.
“Huduma yenu ni muhimu sana kwa uhai wa Sharika, nimeona utofauti mkubwa nilipotembelea Sharika zenye huduma hizi na zisizo kuwa nayo; pia napenda muelewe Dayosisi naKanisa linatambua sana umuhimu wa huduma yenu na ndiyo maana huduma yenu inatambulika katika katiba ya Dayosisi.” Alisema Dkt. Shoo.
Aidha Alisema ni vyema wasiwe na hofu kwa kudhani kwamba huduma wanayofanya haitambuliki wala kuheshimika na kusema Kila mmoja anapaswa kujua huduma yake ni ya muhimu na wala wasikubali mtu yeyote aidharau huduma yenu.
“Kama Neno linavyosema mtambue kuwa huduma hii mmeitiwa na Yesu, na Yesu anatumia njia mbalimbali kutimiza kusudi lake, kwa namna ya kipekee Bwana Yesu alimwita Paulo Katika huduma angali awali alikuwa analitesa kanisa lakini kwa Neema Yesu akamwita akamkabidhi huduma takatifu”
“Na Paulo kwa kutambua kuwa huduma yake aliitwa kutoka na Yesu, aliifanya pamoja na changamoto mbalimbali alizopitia, nanyi mfanye kama Paulo, fanya huduma yako ukitambua Yesu ndiye aliyekuitia kwa kujiamini”
Kadhalika aliwataka kutoshawishika kuwatukuza wanadamu wala kuwapendeza wanadamu katika kazi zao bali wafanye kwa bidii na kwa uaminifu kwa utukufu wa Mungu na Kuzaa matunda mema.
Pia alisema ni vyema wakawa kielelezo katika maisha ya ufuasi wa Yesu na kama kweli ni wafuasi wa Yesu wajiulize kama katika kutenda na kuenenda kwao kunaonekana kama ni wafuasi wa Yesu.
Kwa upande wake Katibu wa Idara ya Wanawake Dayosisi ya Kaskazini Mch. Faustine Kahwa alisema kuwa lengo la kutoa semima imelenga kuwajengea uwezo ili wanapokwenda kwenye sharika zao waweze kutumika kikamilifu.
Na baadhi ya washiki walioshiriki katika semina hiyo Lilian Robinson kutoka Usharika wa natiro amesema kuwa watajifunza mengi ikiwa ni mambo ya Kiroho na ya kimwili.
Wajumbe wa Mkutano Mkuu wa 21 wa KKKT wametakiwa kuhakikisha wanaepukana na masuala ya rushwa katika uchaguzi mkuu wa kumpata Mkuu wa Kanisa hilo unaotarajiwa kufanyika Alhamis ya Agosti 24 , 2023.Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania ambaye pia ni Mkuu wa Dayosisi ya Kaskazini Askofu Dkt Fredrick Onael Shoo, anayemaliza muda wake ametoa onyo hilo Jumanne Agosti 22, 2023 wakati akifungua Mkutano Mkuu wa 21 ambapo wajumbe wanatarajia kufanya uchaguzi wa kumchagua Mkuu wa KKKT.Dkt Shoo amewataka wajumbe hao kutofautisha uchaguzi huo wa mkuu wa Kanisa na chaguzi zinazofanyika sehemu nyingine kwani anae muweka kiongozi yeyote wa Kanisa kwenye mamlaka ni Mungu pekeeAmesema mjumbe yeyote atakae toa au kupokea Rushwa basi fedha hizo ziungue mifukoni mwao.

